Baraza la Vijana Chadema wamelitaka jeshi la polisi nchini kumkamata, William Ngeleja kwa kukutwa na mali ya wizi kutoka (Escrow) na kumuachia Tundu Lissu kwa kusaidia kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu ndege ya Tanzania kukamatwa huko nchini Canada.
Akisoma barua aliyoiandika kwenda kwa Mkuu wa Jeshi la polisi nchini Simon Sirro, na Mkurugenzi wa makosa ya upelelezi mbele ya wanahabari mapema leo jijini Dar es salaam, Mwenyekiti wa BAVICHA, Patrobas Katambi amesema aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Mh. William Ngeleja kupitia pesa alizozirudisha hivi karibuni ni wazi kuwa ni mtuhumiwa ambaye anaweza kutaja wenzake wote kisha wakarudish bilioni 307 ambazo zilichotwa kutoka akaunti ya Tegeta Escrow.
Katambi amesisitiza kwamba hakuna haja ya kumshikilia Lissu pasipokuwa na sababu za msingi kutokana na mamlaka waliyonayo bali wanapaswa kuhakikisha wanawaweka ndani watuhumiwa waliosababishia serikali hasara ya mabilioni ikiwepo kampuni ya Lugumi pamoja na watu waliogawana pesa za Escrow.
"Kumkamata Mhe. Lissu hakuwezi kufanya ndege yetu iliyokamatwa kurejeshwa nchini kwani yeye amewasaidia watanzania kufahamu nini kinachoendelea.
"Sisi ni upinzani tunaopinga na kutoa njia elekezi, katika barua yetu tumemtaka IGP amkamate Ngelleja na wenzake watoe bilioni 307 zetu na Lugumi bilioni 38 kisha wakalipie ndege iliyokamkatwa kwa pesa ya bilioni 87 ili iendelee na kazi lakini siyo kusingizia upinzani kwamba wanapotosha au wanafanya uchochezi.
"Tufanye kama jinsi ilivyokuwa kwenye Biblia kwamba yule mfungwa Baraba aliachiwa huru kisha Yesu akasulubiwa, basi na Lissu tumuachilie kwani hana kosa zaidi ya kuzungumza ukweli na Ngelleja aliyekiri hadharani kwa kurudisha pesa za wizi awekwe ndani na asaidiane na jeshi la polisi.
Pamoja na hayo Mwenyekiti huyo ambaye ni Mwanasheria kitaaluma ameongeza kuwa iwapo jeshi la polisi litashindwa kuwatia nguvuni Mh. Ngeleja na wenzake wao wenyewe watafanya kazi hiyo kwa kutumia sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ya 2002 ijulikanayo kama "Arrest by private person'.
Aidha Katambi amesema kuwa kupitia barua hiyo wasipopata majibu yao watafanya maandamano ya amani nchi nzima ili kuweza kushinikiza haki za kisheria, kiuchumi na kisiasa nazo zifuatwe huku wakiwafundisha vijana namna ya kudai haki zao za msingi.