Wanaoendesha mauaji Kibiti wauawa Mwanza

Watu sita wanaotuhumiwa kujihusisha na uhalifu katika wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji mkoani Pwani wameuawa katika mapambano ya kurushiana risasi na polisi, tukio lililofananishwa na sinema za kivita.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Ahmed Msangi
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Kamanda Ahmed Msangi amethibitishwa kuwapo kwa tukio hilo la alfajiri ya kuamkia jana Mtaa wa Fumagila Mashariki, Kata ya Igoma wilayani Nyamagana huku akisema kuwa kati ya waliouawa, mmoja tu, Selemani Juma ndiye aliyefahamika na wengine watano hawajafahamika majina yao.
Kamanda Msangi amesema majambazi hao walipatikana na silaha aina ya AK 47 yenye namba za usajili 1971E3445 na magazini zake mbili zikiwa na risasi 30 kila moja, silaha nyingine nne zilizotengenezwa kienyeji, na risasi zingine 36 za AK 47 zilizokuwa zimehifadhiwa kwenye begi na sare za jeshi na mikanda yake zinazodaiwa kutumiwa na majeshi ya nchi jirani.
Vitu vingine vilivyokamatwa kwa mujibu wa Kamanda Msangi ni kofia sita za kuficha uso na mabegi matatu yaliyokuwa yamehifadhi risasi, pikipiki moja yenye namba za usajili T 815 DAA aina ya Sanya na baiskeli mbili.
Awali polisi walipokea taarifa kutoka kwa wasiri kwamba baadhi ya wahalifu wanaofanya shughuli za uhalifu katika wilaya za Kibiti na Rufiji mkoani Pwani wamekimbilia mkoani Mwanza na kujificha katika eneo la Fumagila.
Polisi walifanya ufuatiliaji wa haraka wa taarifa hizo katika sehemu mbalimbali za jiji, mkoa wa Mwanza na maeneo jirani na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja ambaye alikiri kufanya uhalifu na kuwapa polisi ushirikiano kwa kuwapeleka hadi eneo la Fumagila ambapo alidai wenzake walikuwa wamejificha huko”, amefafanua Kamanda Msangi.
Kamanda Msangi amesema baada ya polisi kufika katika eneo la Fumagila, ghafla majambazi hao walikurupuka na kuanza kuwarushia polisi risasi, lakini kutokana na umahiri wa askari polisi walijibu mashambulizi na kufanikiwa kuwaua sita huku wawili wakifanikiwa kutoroka kutoka kwenye eneo la tukio.
Hata hivyo Kamanda Msangi amesema kuna taarifa kuwa majambazi waliouawa ndio walioshiriki katika unyang’anyi wa kutumia silaha Juni 15 mwaka huu katika Kiwanda cha mikate cha Victoria, jijini hapa na kupora Sh milioni 30, kisha kukimbilia kusikojulikana ambapo kesi na NY/4747/2017 ilifunguliwa kwa ajili ya tukio hilo.
Chanzo:HabariLeo


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo