Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi Elibariki Kingu, atimiza ahadi yake ya kutopokea Posho yake na kuilekeza Jimboni kwake.
Katika utekelezaji wa azma yake hiyo, mbunge huyo akiwa jimboni kwake jana alitoa misaada yenye thamani ya Sh. milioni 64 kwa wananchi na kueleza kuwa hatarudi nyuma katika azma yake hiyo ya kutozitumia peke yake posho zake za kibunge.
Alisema azma yake hiyo ilichochewa na Rais John Magufuli ambaye mara tu baada ya kuingia madarakani Novemba 5, 2015, alianza kubana matumizi na kuelekeza fedha katika miradi ya maendeleo.
Kingu alisema posho anazopewa mbunge kwa kipindi cha miaka mitano nje ya mshahara ni zaidi ya Sh. milioni 250 ambazo anaamini zinatosha kujenga madarasa, zahanati na vituo vya afya katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa wabunge wote wataridhia kutozielekeza kwenye miradi hiyo.
"Naunga mkono hatua ya Rais kuchukua za kubana matumizi ndiyo maana nimeridhia sehemu ya kipato changu na kupeleka jimboni kwangu kwa ajili ya kutatua changamoto ya elimu, afya, ajira kwa vijana, kina mama na michezo," alisema.
Alisema kuwa huwa anapewa Sh. milioni 47 kwa mwaka kwenye Mfuko wa Jimbo na anajumlisha na posho zake binafsi na kuzielekeza kutatua kero zinazowakabili wananchi wa jimbo lake.
Alisema hatumii hata senti moja kutoka kwenye Mfuko wa Jimbo na posho zake za kibunge badala yake anatumia fedha zake binafsi.
Aliitaja baadhi ya misaada aliyotoa kwa wananchi jana kuwa ni pikipiki 20 zenye thamani ya Sh. milioni 48, vyerehani 10 vya Sh. milioni 3.5, vitanda 40 vyenye thamani ya Sh. milioni 10 na kusaidia vikundi vya kina mama wajasiriamali Sh. milioni tatu kupitia vikundi vyao.
Aliongeza kuwa tangu aingie katika Bunge la 11, ametumia Sh. milioni 119 katika jimbo lake lenye kata 15 kujenga madarasa, ukarabati shule za sekondari za kata, ujenzi wa zahanati na nyumba ya mganga mkuu wa Kata ya Mtunduru.
Alizitaja kata zilizopata fedha hizo kuwa ni Irisya, Sepuka, Mtunduru, Kituntu, Puma, Ihanja, Iseke, Muhintiri, Iyumbu, Makilawa, Minyughe, Ighombwe, Ngungira, Mwaru na Igelansoni.Alisema hadi sasa amefanya maendeleo makubwa kwa kata hizo kwa kujenga zahanati na kujenga madarasa mapya kwenye jimbo hilo la Singida Magharibi.
Kingu aliongeza kuwa ameanzisha ujenzi wa shule mpya za msingi jimboni kwake ili kuwasaidia wanafunzi wanaotembea umbali mrefu wa zaidi ya km 10 kupata huduma hiyo.
Alizitaja shule hizo mpya kuwa ni Utaho, Winduwindu, Mtakuja iliyopo kata ya Mwaru, Mtunduru, Mwankhalaja, Mfumbuahumba, na Magwaghana.
Mbunge huyo pia alisema zahanati mpya zimeanza kujengwa kila kijiji akieleza kuwa anajivunia mradi huo kwa kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ya chama chake (CCM).
Hafla ya utoaji vifaa hivyo ilihudhuriwa na Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson pamoja na viongozi wengine wa kiserikali na wabunge waliofika jimboni kwa mbunge huyo kumuunga mkono.
Awali akitangaza kutochukua posho hizo 2015, mbunge huyo alisema: "Ili niwe na uhalali wa kuikemea serikali ya chama changu cha CCM katika matumizi yasiyo ya lazima, inabidi nianze mimi kwa kutochukua fedha zozote za posho (sitting allowance) wakati wote wa Bungekwa miaka mitano.
"Tayari nimemwandikia Katibu wa Bunge kwamba kwa miaka mitano posho zote ambazo ni zaidi ya Sh. milioni 200 hazitapita kwenye mifuko yangu bali hospitalini, watoto wanaokosa madawati na kuboresha miundombinu.
"Kwa dhamira safi tukiamua kubana posho mimi na wabunge wenzangu tutafika mbali na ninaomba wabunge wenzangu wanisapoti. Nimeona sina sababu ya kuchukua posho kwa sababu ninalipwa mshahara.
"Sitakuwa wa kwanza kupinga kuchukua posho kwa kuwa kuna watu tayari walianza kuonyesha pia nia hiyo akiwamo Zitto Kabwe (Mbunge wa Kigoma Mjini, ACT-Wazalendo), ninaamini wabunge wataonyesha uzalendo.
"Kama jambo hili la kukata posho kwa wabunge litatekelezwa, ni dhahiri tutafika mbali. Bunge lina jumla ya wabunge 394, vikao vya Bunge kisheria kwa mwaka ni wastani wa vikao 140 mpaka 180. Sasa kila mbunge akilipwa Sh. 220,000 kila siku kwa wabunge 394, ukipiga hesabu kwa miaka mitano, utaona ni kiasi gani cha fedha kitaokolewa."
POSHO 340,000/- KWA SIKUNipashe inafahamu kwamba kila mbunge analipwa mshahara wa Sh. milioni 3.6 kwa mwezi.
Pia Mei 17, mwaka jana, Dk. Tulia aliiambia Nipashe kuwa kila mbunge analipwa posho ya Sh. 220,000 kwa siku (Sh. 110,000 kikao cha asubuhi na kiasi hicho kikao cha jioni) na anapewa pia Sh. 120,000 kila siku kwa ajili ya chakula na malazi kunapokuwa na shughuli za chombo hicho.