Askari walioagizwa kumtoa, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika bungeni Ijumaa iliyopita, wamepangiwa vituo vingine vya kazi kwa kuchelewa kutekeleza agizo la Spika.
Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema aliwashangaa askari hao kwa jinsi walivyokuwa wanambeleza mbunge huyo wa Kibamba kutoka nje.
"Askari hawa wataendelea kuhamishwa mpaka pale tutakapowapata wanaofaa," amesema Ndugai.
Mnyika alitolewa bungeni Ijumaa iliyopita baada ya mmoja wa wabunge kusema ‘Mnyika mwizi’ akimhusisha na wizi wa madini.
Kutokana na hali hiyo Mnyika alimtaka Spika kuchukua hatua dhidi ya mbunge aliyesema kuwa yeye ni mwizi lakini Spika alisema hajui hilo na haijaingia kwenye hansadi.
Hata hivyo Mnyika alisisitiza kuwa mambo hayawezi kwenda hivyo.
Baada ya majibizano kati yao Spika aliamuru walinzi wamtoe Mnyika nje ya Bunge.