Mbunge Matatani Kwa Kumtukana Mwandishi wa Habari aliyekuwa akimhoji

MBUNGE wa Gatundu Kusini Moses Kuria (pichani) Jumanne alikabiliwa vikali na Wakenya mitandaoni baada ya kumtusi mwanahabari Kennedy Mureithi wa runinga ya NTV Kenya kwa kumwita “mshenzi.”

Bw Kuria alikuwa akihojiwa kuhusu utaratibu wa mchujo wa Chama cha Jubilee katika eneobunge lake, wakati alichemka na kutoa matamshi hayo.

Aidha, alikasirishwa na Bw Mureithi, alipomuuliza kuthibitisha ikiwa ni kweli kwamba amekuwa akitumia vitisho dhidi ya baadhi ya wawaniaji wa wadhifa huo.
Hilo linatokana na kisa cha wiki iliyopita, ambapo gari moja lilinaswa katika eneobunge lake likiwa limebeba mapanga, ambayo haikubainika mara moja yalikokuwa yakisafirishwa.
Hata hivyo, mbunge huyo alikasirishwa na swali hilo, akimtaka mwanahabari huyo kumpelekea wawaniaji ambao wamenukuliwa wakitoa matamshi hayo.
“Wako wapi wawaniaji ambao unadai wanasema kwamba natumia mbinu chafu kuwatishia? Nimechoshwa na uanahabari duni! Mshenzi!” alisema mbunge huyo, huku akiondoka katika mahojiano kighafla.
Bw Kuria alidai kwamba vyombo vya habari vimekuwa vikimwonea kwa kila maonevu yanayofanyika, akitaja hilo kama uwepo wa “nia mbaya dhidi yake.”
“Kila jambo mbaya linalofanyika ninalaumiwa kwalo. Hii ni njama ya wazi ya kuniharibia sifa,” akafoka Bw Kuria.
Kumekuwa na madai kwamba gari hilo lilihusishwa na Bw Kuria, hasa baada ya karatasi zilizokuwa na picha zake kupatikana zikiwa katika gari hilo.
Hata hivyo, amekanusha madai hayo, akishikilia kuwa njama hiyo ilipangwa na washindani wake kisiasa ili kuhakikisha anashindwa kwenye zoezi la mchujo.
Hicho si kisa cha kwanza kuhusisha na mbunge huyo mbishani, kwani si mara moja ametoka ghafla katika mahojiano.
Mwaka uliopita, aliondoka studioni, wakati akihojiwa na mwanahabari Hussein Mohammed wa runinga ya Citizen kuhusiana na kisa ambapo alinaswa katika video akitoa matamshi ya uchochezi kwa vijana aliodai kuwa “jeshi” lake.
Kwenye video hiyo, aliyodai kuwa ilikuwa imehaririwa ili kumharibia jina, Bw Kuria aliwaambia vijana hao kumkata yeyote ambaye anapinga miradi ya maendeleo iliyokuwa ikiendeshwa na Huduma ya Kitaifa kwa Vijana (NYS).



JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo