Manara Yamfika, Afungiwa Soka na Faini ya Mamilioni Juu


Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM

KAMATI ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imemfungia Hajji Manara, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba kwa mwaka mmoja kutojihusisha na masuala ya soka pamoja na kumpiga faini ya Sh. Milioni 9.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu, Wakili Jerome Msemwa amewaambia Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam kwamba hatua hiyo imefikiwa baada ya Manara kukutwa na makosa matatu dhidi ya TFF waliomlalamikia.

Msemwa ameyataja makosa hayo ya Manara dhidi ya mlalamikaji, TFF ni kuituhumu na kuidhalilisha TFF, kueneza chuki za ukabila na la tatu kuingilia utendaji wa shirikisho hilo.

Kwa makosa hayo yote, anakumbana na adhabu ya kuwa nje ya masuala ya soka kwa mwaka mmoja na kulipa faini ya Sh. Milioni 9 kabla ya kumaliza adhabu yake.



Kosa la kwanza amehukumiwa kwa mujibu wa kanuni ya 41 kifungu cha tisa ambalo alitakiwa alipe faini ya Sh. Milioni 1, la pili amehukumiwa kwa kanuni ya 53 kifungu cha kwanza na cha pili na anafungiwa miezi mitatu na faini ya Sh. Milioni 3 na kosa la tatu amehukumiwa kwa kanuni ya kwanza na ya pili inayohusu Maadili, ambayo alitakiwa afungiwe miaka saba na faini ya Sh. Milioni 5.


Lakini kutokana na kuwa hilo ni kosa lake la kwanza Kamati imetumia mamlaka yake kwa kumpunguzia adhabu hadi miezi 12 na faini ya Sh. Milioni 5 – na adhabu hizo zimeunganishwa, hivyo atatumikia kifungo cha mwaka mmoja na kulipa faini ya Sh. Milioni 9.

Hata hivyo, Msemwa alisema Manara hakutokea kwenye kikao cha kutoa utetezi wake dhidi ya tuhuma hizo, ingawa taarifa ya kuitwa alifikishiwa yeye na klabu yake pia. 

Adhabu hii inafuatia Manara ‘kuishambulia’ TFF    
Katikati ya wiki, Manara aliituhumu TFF kufanya njama za waziwazi ili kuwabeba wapinzani wao, Yanga katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Manara pia aliwatuhumu viongozi wakuu wa TFF, Jamal Malinzi na Katibu wake, Selestine Mwesigwa ni wahaya na viongozi wa zamani wa Yanga, ambao wanataka kuipendelea Kagera Sugar na timu hiyo yao hiyo ya zamani.

Na hamaki ya Manara, ilifuatia TFF kulipeleka Kamati ya Katiba Sheria na Hadhi za Wachezaji suala la Simba kupewa ushindi wa zamani na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi Tanzania, maarufu kama Kamati ya Saa 72.

Kamati ya Saa 72 iliipa Simba SC pointi tatu na mabao matatu baada ya kujiridhisha beki wa Kagera Sugar, Mohammed Fakhi aliichezea timu hiyo dhidi Wekundu wa Msimbazi Aprili 2, mwaka huu akiwa ana kadi tatu za njano, ambayo ni kinyume cha kanuni.

Lakini siku mbili baadaye, Kagera Sugar wakapinga maamuzi hayo na kuomba suala hilo lisikilizwe upya kwa kuwa mchezaji wao hakuwa na kadi tatu za njano siku wanaifunga Simba 2-0 Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

Bonyeza hapo chini Usikilize sauti ya tukio hilo mwanzo mwisho>>>>>>

Chanzo:Bin zubeiry


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo