Wazazi na walezi wilayani Makete mkoani Njombe
wameshauriwa kujitokeza kwa wingi kuwapatia chanjo watoto wao katika
maadhimisho ya wiki ya chanjo duniani
Akizungumza na mwandishi wetu ofisisni kwake, Mratibu wa
shughuli za Chanjo katika halmashauri ya wilaya ya Makete Bw. Felician Chawala
amesema kiwilaya maadhimisho hayo yatafanyika katika kijiji cha Ndulamo kata ya
Iwawa wilayani hapa kuanzia Aprili 24 hadi Aprili 30 mwaka huu huku mgeni Rasmi
akitarajiwa kuwa Mkuu wa wilaya ya Makete
Amesema wilaya ya Makete haiko nyuma katika utekelezaji
wa maadhimisho hayo na kusema wamejipanga kikamilifu kuhakikisha maadhimisho
hayo yanafanyika kama ilivyopangwa
Bw. Emilian Mbijima ni Mratibu wa afya ya uzazi na mtoto
Halmashauri ya wilaya ya Makete amesema ni muhimu kwa wazazi wote wawili baba
na mama wakatambua umuhimu wa mtoto kupatiwa chanjo, hasa baba kwa kuwa
itasaidia kumkumbusha mama pale anapokuwa amesahau wakaongozana kwa pamoja
kumpeleka mtoto wao kupatiwa chanjo
Amesema ni furaha kwao wataalamu wa afya kuona jamii
inaelewa umuhimu wa chanjo kwa watoto kwa kuwa inasaidia kuwakinga na maradhi
mbalimbali pamoja na kuepusha vifo ambavyo vingetokana na watoto kutopatuiwa
chanjo
Maadhimisho hayo yanaongozwa na ujumbe usemao "Chanjo
hukinga kila mtu, pata chanjo" huku kaulimbiu ya mwaka huu ikisema "Jamii
iliyochanjwa ni jamii yenye afya"
