Mwigulu: Aliyemtolea Bastola Nape akamatwe


Kufuatia tukio la mtu mmoja aliyedaiwa kuwa ni Askari kumtishia Mbunge Nape Nnauye kwa kutumia bastola, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi amesema tukio lile halikuwa sahihi na kuagiza hatua zichukuliwe.

Waziri Mwigulu Nchemba ambaye ndiye mwenye dhamana ya kusimamia usalama wa raia na mali zao amesema kuwa, Nape Nnauye si jambazi, hakuwahi kuwa na taarifa za uhalifu, sasa kwanini mtu amtishe kwa bastola tena mbele ya umati mkubwa uliojaa waandishi wa habari?

“Mh.Nape Moses Nnauye sio jambazi, ni mtanzania, ni mbunge, mjumbe wa NEC wa CCM, hana record ya uhalifu. Kitendo cha mtu kumtolea Bastola, Sio cha kiasikari, sio cha kitanzania na sio cha ki Mungu, kama mtu ameweza kutoa Bastola mbele ya Kamera nawaza mbali ingekuwa kwenye uchochoro angefanya nini.”

Aidha, Waziri Nchemba amesema kuwa amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Ernest Mangu kumbaini mtu huyo aliyefanya kitendo hicho na kumchukulia hatua stahiki.

“Nahusika na Usalama wa Raia wote wa Tanzania, nimemwelekeza IGP atumie picha kumsaka mtu yule aliyeinua kufanya kitu cha kihalifu kwa kofia ya uaskari. Na kama ni Askari basi sheria zinazoongoza taasisi husika zichukue mkondo wake.”


Nape Nnauye alitishwa na bastola hiyo jana alipofika katika Hoteli ya Protea Dar es Salaam kwa lengo la kuzungumza na waandishi wa habari baada ya Rais Dkt John Pombe Magufuli kumvua Uwaziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo