MAKACHERO wa Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro, bado wanaendelea kumtafuta mtuhumiwa wa mauaji ya kukusudia ya kada wa Chadema, Anitha Kimario (44), ambaye aliuawa kwa kunyongwa na watu wasiojulikana na kisha kuzikwa nusu katika mashamba ya miwa.
Kada huyo ambaye pia alikuwa mfanyabiashara wa Jiji la Dar es Salaam, aligombea ubunge wa Viti Maalum Wilaya ya Hai, katika uchaguzi mkuu uliopita.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Wilbrod Mutafungwa, mtuhumiwa anayetafutwa ataunganishwa na wenzake watatu ambao wanadaiwa kukiri kosa la kumuua kada huyo.
Aliuawa Machi 2, mwaka huu na mwili wake kuokotwa ukiwa umevuliwa nguo na kutupwa katika matuta ya kuoteshea miwa, karibu na Kiwanda cha Sukari cha TPC, Wilaya ya Moshi.
“Bado tunahangaika kumtafuta mtuhumiwa mmoja muhimu wa mauaji hayo, lakini askari wangu wameweka mitego ya kila namna kuhakikisha kwamba tunamtia mbaroni kama tulivyowapata hawa wengine watatu ambao wamekiri kosa,” alisema.
Kati ya watuhumiwa waliokamatwa, yumo mtu na mpenzi wake ambao ni Wilfred Mauga (31), maarufu rasta, mkazi wa Mount Meru Arusha na Esther Shirima (31), na Wilfred Silayo (41), mkazi wa Manispaa ya Moshi.
Inadaiwa kuwa Mauga au rasta ambaye ni mpagazi, anadaiwa kumpigia simu mara ya mwisho marehemu Anitha na kumtaka aende Moshi mjini ili waonane. Pia inadaiwa alikuwa akidaiwa na marehemu Shilingi milioni tano.
Anitha alipotea katika mazingira ya kutatanisha Februari 27, mwaka huu, baada ya kuondoka nyumbani kwake Tarakea, Wilaya ya Rombo na kuaga anaelekea mkoani Arusha kudai madeni yake ya kibiashara.
Kabla ya mauaji hayo, Machi mosi, mwaka huu, makachero wa polisi walilikuta gari la marehemu huyo aina ya Toyota RV4 yenye namba za usajili T 728 CEW, rangi nyekundu ikiwa imetelekezwa eneo la Bomambuzi, Manispaa ya Moshi, huku milango yake ikiwa imefunguliwa na funguo za gari zikiwa kwenye swichi.