Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Mhe. Jaji (R) Semistocles Kaijage amewataka watumishi wa tume hiyo wazingatie maadili na kanuni za utawala bora ili kutekeleza kwa ufanisi jukumu la Tume katika kukuza na kuimarisha demkorasi na utawala bora nchini.
Jaji Kaijage ameyasema hayo alipoalikwa kuwa mgeni rasmi kufungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Tume kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima jijini Dar es Salaam.
“Jukumu kubwa la Tume ni kukuza na kuimarisha demkorasi na utawala bora nchini, kwa maana hiyo ni muhimu kwamba watumishi wa Tume wazingatie maadili na kanuni za utawala bora ili kutekeleza kwa ufanisi jukumu hili” alisema na kuongeza kuwa:
“Ni muhimu kwa watumishi wa Tume katika utendaji kazi wao kuepuka vitendo vya ukiukwaji wa maadili kama vile rushwa, upendeleo na au ubaguzi wa aina yoyote katika sehemu ya kazi”
Mbali na hayo, Mhe. Jaji Kaijage aliipongeza Tume kufanikisha uchaguzi mdogo uliofanyika mwezi Januari mwaka huu katika jimbo la Dimani na kata 20 za Tanzania Bara kwa kuufanya kuwa wa amani na utulivu pamoja na changamoto mbalimbali zilizoukabili uchaguzi huo.
Mbali na kutoa maelekezo hayo Mgeni rasmi huyo wa ufunguzi wa kikao cha Baraza la wafanyakazi wa NEC, alitoa wito kwa wajumbe wa kikao hicho na watumishi wote wa Tume kuitafsiri kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu kwa vitendo na kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali.
Alieleza matumaini yake juu ya umoja na ushirikiano uliopo Tume kwamba vitaimarika na kuwa taasisi hiyo itatekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kujenga nguvu na mshikamano wa pamoja kwa wafanyakazi wote.
Katika kikao hicho cha siku mbili mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo Mapitio ya mwaka 2016/2017 na Makisio ya Bajeti ya mwaka 2017/2018, Wajibu wa Mtumishi, Dawa za Kulevya na Athari zake kwa jamii na Namna ya Kupambana na Ugonjwa wa Ukimwi.
“Ninaomba mjadili mada hizo kwa kina na busara mkitambua kuwa matokeo ya majadiliano yenu ni kwa ajili ya maslahi ya Tume na taifa kwa ujumla” alisema Mhe. Jaji Kaijage na kufafanua kuwa:
“Kwa kuwa kipind hiki ni cha bajeti nashauri na kusisitiza mjadili kwa kina vipaumbele vya bajeti vya taasisi ili viwe ni msingi wa kuiwezesha Tume kuwa na ubunifu na uthubutu wa kuibua mawazo mapya yatakayoiwezesha kupiga hatua zaidi na utendaji kazi bora wa kila siku”
Aliwakumbusha wajumbe kuwa mabaraza ya wafanyakazi yameundwa kwa mujibu wa Waraka wa Rais Namba 1 wa mwaka 1970 na moja ya madhumuni ya kuanzishwa kwake ni kuongeza ufanisi na tija kazini.
Aliongeza kuwa kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma toleo namba 3 la mwaka 2009, limefafanua kuwa lengo ni kutoa uwanja wazi wa majadiliano kati ya watumihsi na waajiri katika kutoa maamuzi katika masuala ya ajira.
Hivyo aliwawaomba wajumbe wa baraza la wafanyakazi la Tume watumie fursa ya kikao hicho kuwawakilisha wafanyakazi wenzao vizuri kwani vikao vya baraza ni sehemu muhimu ya kujadili namna ya kuboresha mazingira ya kazi na kutimiza malengo yake.
“Uzoefu unaonesha kuwa mabaraza ya wafanyakazi yanapotumika vizuri hali ya maelewa na utulivu sehemu za kazi huongezeka na hivyo kuongeza tija kazini” alisema.
Akimkaribisha mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC Bw. Kailima Ramadhani, mbali na kuwambusha wajumbe lengo la kuanzishwa mabaraza ya wafanyakazi, alisema baraza pia lina wajibu wa kutoa maagizo mbalimbali kwa ajili ya kuboresha na kutekeleza malengo ya taasisi.
Aliongeza kuwa baraza pia ni eneo ambalo mwajiri anapaswa kutoa ufafanua kwenye maeneo ambayo watumishi watahitaji kupata ufafanuzi hasa kuwasilisha mapendekezo ya mwelekeo wa Bajeti ya Taasisi kabla haijawasilishwa kwenye Kamati ya Bunge.
Wakati akimshukuru mgeni rasmi kwa ufunguzi, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (Tughe) Taifa Bw. Heri Mkunda alimueleza mgeni rasmi jinsi anavyoridhishwa na jinsi baraza la wafanyakazi linavyopewa umuhimu na Tume.
Bw. Mkunda pia alimpongeza Mhe. Jaji Kaijage kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume na kwamba Tughe Taifa wana imani naye atatimiza vyema ujenzi wa demokrasia nchini na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwake ili kutimiza lengo hilo.