Kwa mujibu wa mdhamini wa ndoa iliyokuwa iliyotarajiwa kufungwa mwishoni mwa wiki iliyopita, alifahamika kwa jina moja la Lomboi, alisema tukio hilo lilitokea mwishoni mwa wiki.
Alisema, Sarah Sumaye (26), ambaye ni mtoto wa Mchungaji Yosia Sumaye, amemwacha mchumba na ndugu zake katika masikitiko makubwa.
“Alitoroka wakati mke wangu anamuandaa kumpeleka salon kwa ajili ya maandalizi ya ndoa, na ndoa hiyo ilitarajiwa kufungwa katika Kanisa la Elim Pentekoste lililopo Babati mjini,” alisema.
Ilidaiwa kwamba bibi harusi mtarajiwa alitoka nje kwa ajili ya kufanya usafi wa kinywa na meno na tangu wakati huo hadi sasa hajulikani alipo huku akiwaacha ndugu na jamaa katika wasiwasi mkubwa.
Nipashe ilipofanya jitihada za kumpata baba yake na binti huyo hazikuzaa matunda, lakini mdhamini wake alisema baada ya tukio hilo baba ya binti alienda mochwari kwa ajili kuona kama ameuawa.
Wazazi wa kijana na bwana harusi hawakuweza kuonekana, huku taarifa zilizotolewa na msimamizi wa ndoa zikidai kuwa bwana harusi alipelekwa Mererani kwa ajili ya mapumziko ili kuondoa msongo wa mawazo.
Hali kadhalika inasemekana kuwa bwana harusi aliwahi kupigiwa simu na kijana mmoja asiyemfahamu na kumtolea vitisho huku akimwambia ndoa hiyo haitafanikiwa kufungwa.
Alipoulizwa kwa njia ya simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Francis Massawe, alisema hana taarifa hiyo, lakini polisi watafuatilia kubaini alipo.