ASKARI wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Said Hashimu (30), amefariki dunia baada ya pikipiki aliyokuwa akisafiria kugongana uso kwa uso na gari eneo la mlima Pasua barabara ya Kigoma-Kasulu, Manispaa ya Kigoma/Ujiji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Ferdinand Mtui, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 10:00 jioni.
Kamanda Mtui alifafanua kuwa gari lenye namba za usajili T888 BSB aina ya Nissan lililokuwa likiendeshwa na David Mashauri (47), mkazi wa Wilaya ya Kibondo, liligongana uso kwa uso na pikipiki yenye namba za usajili MC 271 BFV aina ya Kinglion na kusababisha dereva wa pikipiki hiyo, Hashimu (30) ambaye ni askari wa JWTZ kufariki dunia papo hapo.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa gari hilo.
Aidha, Kamanda Mtui alisema dereva Mashauri ametiwa mbaroni na upelelezi ukikamilika, atafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.
Aliwataka madereva wa vyombo vya moto kutii sheria za usalama barabarani ili kuepukana na vifo pamoja na majeruhi kutokana na ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani.