SINTOFAHAMU ya aina yake imewakumba wafanyakazi wa Halmashauri ya Morogoro waliohamia eneo la Mvuha, kama agizo la serikali lilivyowataka, baada ya Kamati ya Fedha na Mipango ya Baraza la Madiwani, kusema shughuli zihamie maeneo mbalimbali, ikiwamo Matombo.
Wakati Mkurugenzi Mtendaji (DED) wa Halmashauri hiyo, Sudi Mussa Mpili akisema kwamba amri ya kuhamia Mvuha inabaki palepale kama serikali kuu ilivyoagiza, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Kibena Kingo alisema hawapingi kuhamia Mvuha, bali eneo halistahili kwa kukosa miundombinu.
Mwenyekiti huyo alisema kwamba pamoja na Mkurugenzi kuhamisha watu wake wote kuwa Mvuha Desemba 27, eneo hilo halikidhi mahitaji, likiwa halina umeme na pia likiwa na nyumba chache za watumishi, hali ambayo anasema itafanya shughuli za kitawala zisifanyike.
Kibena alisema suala si kuhamisha, bali suala ni kama watendaji wanaweza kutoa huduma katika mazingira ya eneo hilo.
Alisema baada ya agizo la kuhamia Mvuha, waliitisha kikao cha Kamati ya Fedha na Mipango ya baraza la madiwani, ambayo ilishauri kuwa kuwepo na mtawanyiko wa idara za halmashauri hiyo ili kazi ziweze kufanyika.
Kibena alisema katika mtawanyiko wao huo, wanapeleka idara katika maeneo ya Tawa, Matombo, Morogoro Mjini na Mvuha penyewe. Alisema wanamtaka DED akakae Matombo, eneo ambalo wanaona lina nyumba za kutosha na pia kuna umeme.
Hata hivyo, akihojiwa na gazeti hili alisisitiza kwamba amri ya kuhamia Mvuha ipo palepale. Pia alisema anajaribu kuelimisha madiwani hao, kufuata makubaliano ya awali ya kuhamia Mvuha, kama serikali kuu inavyotaka, badala ya kutawanya ofisi hizo.
Alisema pamoja na kuleta dhiki katika utendaji, itakuwa ngumu kusimamia watendaji waliotawanyika maeneo tofauti yenye umbali mkubwa, kama madiwani hao wanavyopendekeza. Kwa upande wao, walipohojiwa, wafanyakazi walisema kitendo cha kuwahamishia Mvuha na kisha kuwataka tena waondoke huko kwenda maeneo mengine ni cha usumbufu mkubwa.
Walisema walikwepa kuleta mgongano na serikali kuu, hivyo walikubalia kuhamia hapo na wengine walishalipa kodi ya pango. Mmoja wa wafanyakazi aliyewasiliana na gazeti hili, ambaye hakutaka jina lake liandikwe, alisema kwamba wamehamia hapo bila fedha kutoka kwa mwajiri na kutumia fedha zao kujipatia makazi.
“Hatuwezi kuelewa hili la kurejeshwa Morogoro na wengine kutawanyika maeneo mbalimbali. Tumefika hapa wenyeji wametupatia makazi kwa malipo ya kodi ya pango ya shilingi 50,000 kwa mwezi kwa miezi sita, sasa nani atalipa hizi fedha,” aliuliza mfanyakazi huyo.
Kikao cha Desemba 30 cha kilitaka wafanyakazi kuhamia Mtamba, ambako imeelezwa kuwa hakuna eneo la ofisi inayoweza kukidhi mahitaji kwa kulinganisha na Mvuha ambako yako majengo ya serikali.
Desemba 23 mwaka huu serikali ilitoa tamko Mvomero, ikitaka watendaji kuhamia Mvuha na kwamba kama madiwani watakataa atavunja baraza, kwani muda mrefu umepita na wananchi hawapati huduma. Halmashauri ya Morogoro ni moja ya halmashauri za zamani, zilizoundwa wakati wa kurejeshwa kwa mamlaka za mikoa mwaka 1992.
Halmashauri hiyo imekuwa na migongano mingi ya maeneo ya kuwekwa kwa makao makuu ya halmashauri. Migongano hiyo ilikuwa moja ya sababu ya kumegwa kwa wilaya ya Mvomero, ambayo ilikuwa sehemu ya wilaya ya Morogoro, ambayo ipo halmashauri ya Morogoro.
Ingawa umegaji huo ulisababishwa na ukubwa wa wilaya, ambayo kipindi hicho ilikuwa na kata 40. Ingawa Mwenyekiti wa halmashauri alikana kuwapo kwa migongano ya eneo linalostahili kuwa makao makuu, kukubali kwa Baraza katika kikao cha Desemba 26 kuhamia Mvuha na Mkurugenzi kuhamisha watu wake Desemba 27 na wao kuketi kama kamati kutoa mapendekezo mapya, kunaonesha hali katika halmashauri hiyo sio shwari.
Mwenyekiti wa halmashauri alipoulizwa swali kwamba kama ilikuwa inajulikana Mvuha kuna tatizo, kwa nini hawakupendekeza eneo jipya katika siku za nyuma, alisema yeye anayo taarifa inayoonesha tatizo la Mvuha, lakini kwa sasa ndio wanaitisha baraza kamili kutoa maamuzi.
Alifafanua kwamba tangu awali eneo la Mvuha limekuwa na matatizo, hasa kutokana na kubainika kuwa maji yako karibu na uso wa ardhi. Alisema kwamba si sahihi kuweka makao makuu eneo hilo. Hata hivyo, hakusema kwa miaka yote hiyo tangu eneo hilo lipangwe kama makao makuu ya halmashauri, kwanini hawajafanya kikao cha kushauri kubadilishwa kwa eneo.
“Sasa ndio tunataka kukaa baraza zima baada ya mapendekezo ya Kamati ili tupeleke mapendekezo yetu. Lakini kwa sasa tunataka DED abaki Matombo na baadhi ya watu wengine waende maeneo mengine, Mvuha tunakwamisha utendaji wa kazi,” alisisitiza.
Mwenyekiti huyo ambaye ni Diwani wa Ngerengere, alisema mapendekezo yao yana maana kubwa. Katika kuthibitisha kwamba kamati hiyo haikukurupuka, Kibena alisema kwamba alikuwa na mazungumzo na Mkuu wa Mkoa, Kebwe Steven Kebwe ambaye aliwataka kuangalia inavyowezekana na wasikwamishe kazi za serikali na kwamba mpango huo wa kutawanya idara, ameuafiki.
Juhudi za kumpata Mkuu wa mkoa kwa jana hazikuweza kufanikiwa. Wafanyakazi ambao wameshalipia miezi sita kupata makazi, walisema wanashindwa kuelewa wafanye nini, kwani tayari wengine wameshapewa taarifa na wakubwa wao kurejea katika majengo ya zamani ya halmashauri ya mjini Morogoro.
Mpili alisema kwamba utekelezaji wa maagizo ya baraza ni mgumu kwa halmashauri hiyo yenye tarafa sita za Mvuha, Mikese, Ngerengere, Mkuyuni, Matombo na Bwakila Chini. “Mimi nadhani haifai kulumbana katika hili, serikali imeagiza tutekeleze, mwenendo wa baraza unaniweka katika hali ngumu sana ya kiutawala,” alisema Mpili.
Aliongeza kuwa, “huwezi kupeleka ofisi ya Afya Tawa, DED akae Mvuha, idara ya kilimo na mifugo ikakae Matombo, Utumishi na Tasaf warudi mjini, Sheria ikae Matombo hii haiwezekani.”
Kwa mujibu wa DED, makubaliano ya kuhamia Mvuha, yalifikiwa na pande zote za utawala katika kikao ambacho pia mkuu wa mkoa alikuwepo. Alisema ni vyema kuanza na changamoto zingine zitaangaliwa.
Kuhusu tatizo la umeme, Kibena alikiri kwamba umeme wa REA umefika, tatizo ni kwamba haujawashwa. Alisema kwamba makao makuu ya halmashauri, hayawezi kukaa mahali ambapo hakuna umeme. Alisema adha nyingine ni kukosekana kwa makazi kwa watendaji.
chanzo: Habarileo