Mtu wa kiume ambaye hajatambulika mara moja jina lake
anayetuhumiwa kwa wizi wa mifugo ameuawa kwa kuchomwa moto mpaka kufa katika
kijiji cha Ugabwa kata ya Lupalilo wilayani Makete usiku wa kuamkia leo
Kwa mujibu wa wananchi waliozungumza na mwandishi wetu
eneo la tukio, wanasema limetokea leo usiku kati ya saa 7 na saa 8, ambapo
watuhumiwa hao walikuwa wawili wakiwa na mbuzi wawili waliokuwa wamewabeba
kwenye tenga wakiwa wamepakizana kwenye pikipiki, ndipo watu ambao hawafahamiki
walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja na kumuua kwa kumchoma moto yeye pamoja
na pikipiki inayodaiwa kutumika katika tukio la wizi wa mbuzi hao
Mwananchi aliyejitambulisha kwa jina la Nyamo Sanga
ambaye amesema mbuzi hao ni wa kwake, akizungumzia tukio hilo amesema aliamshwa
na mwenyekiti wa kijiji usiku majira ya saa 8 na walipofika eneo la tukio
walikuta moto ukiwaka na kuogopa kusogelea eneo hilo mpaka ulipozimika na
ilipofika alfajiri aliweza kuwagundua mbuzi waliokuwa wamefungwa pembezoni mwa
mwili wa marehemu wanaodaiwa kuwa wameibiwa kuwa ni wa kwake
Mkazi mwingine wa kijiji hicho Bi Anahuruma Amulike
amesema taarifa za kutokea kwa tukio hilo amezipata asubuhi baada ya kuamshwa
na jirani yake huku akisisitiza kwamba tukio hilo ni baya na haungi mkono
kitendo cha wananchi kujichukulia sheria mkononi, na wale wenye tabia kama hizo
waache na wajishughulishe na shughuli halali za kuwapatia kipato
Mzee Daudi Vilumba ambaye nyumba yake iko mita chache
kutoka lilipotokea tukio hilo amesema alilisikia kelele wakati likitokea na
kutokana na uzee wake walifanya jitihada za kuujulisha uongozi wa kijiji kwa
kushirikiana na mkewe
Mwenyekiti wa kijiji hicho Bw. Obadia Sanga akizungumza
na mwandishi wetu eneo la tukio amesema tukio hilo ni mara ya kwanza kutokea
katika kijiji chake na ameelezea mazingira ya kutokea kwake
Nikolaus Andrea Sanga ni Afisa mtendaji wa kijiji hicho
ambapo ameelezea hatua alizozichukua yeye kama kiongozi wa serikali kijijini
hapo mara baada ya tukio hilo ikiwemo kutoa taarifa kwa jeshi la polisi
Akithibitisha kifo cha marehemu huyo Daktari Tabibu
kutoka hospitali ya wilaya ya Makete Traiphon Mayala ameelezea sababu za kifo
cha marehemu baada ya kuufanyia uchunguzi mwili wake kuwa alipigwa na vitu
mbalimbali mwilini mwake vilivyosababisha majeraha na kuvuja damu nyingi na
kufariki dunia ndipo akachomwa moto
Jeshi la polisi Makete limefika eneo la tukio na kuchukua
taarifa za mauaji hayo na kuruhusu mwili huo ambao umeungua kiasi cha
kutotambulika uzikwe