Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi iliyopo wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro imewataka wafugaji wa wilaya tano za mikoa ya Kilimanjaro na Tanga kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria askari wake watakaobainika kuwapiga wafugaji watakaokutwa na mifugo yao ndani ya hifadhi hiyo na kusababisha migogoro ya mara kwa mara.
Mhifadhi mkuu wa Mkomazi Bw Marco Meoli ametoa tamko hilo kufuatia malalamiko ya wafugaji katika mkutano kati ya viongozi wa wafugaji kutoka wilaya za Same, Mwanga, Korogwe, Lushoto na Mkinga na viongozi wa wilaya hizo kujadili changamoto zinazowakabili kati ya pande hizo na jinsi ya kuzipatia ufumbuzi.
Bw Meoli amesema, ofisi yake haijapokea malalamiko rasmi ya askari wake kuwapiga na kuwadhalilisha wafugaji ambacho ni kinyume cha sheria kwa askari hao kupiga wafugaji wanachotakiwa kufanya ni kuwatoza faini mifugo yao inapoingizwa ndani ya hifadhi.
Akizungumza katika mkutano huo uliowajumuisha wakuu wa wilaya na wabunge wa wilaya hizo mkuu wa wilaya ya Korogwe Mhandisi Robert Gabriel amesema, chanzo cha migogoro mingi kati ya pande hizo ni baadhi ya viongozi wa serikali za vijiji na baadhi ya askari wasio waaminifu Mkomazi ambao wamewageuza wafugaji kuwa mitaji yao.
Naye mkuu wa wilaya ya Same ambaye alikuwa mwenyekiti wa mkutano huo Bi Rosemary Senyamule amezitaka pande zote kutekeleza agizo la serikali la kuweka mipaka kati ya vijiji na hifadhi hiyo ili kuondoa migogoro kati ya pande hizo.
Hata hivyo meneja wa ujirani mwema wa Tanapa Bw Ahmed Mbugi amesema, kwa zaidi ya miaka kumi iliyopita Tanapa imetumia zaidi ya shs. 30.6bil/= kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa vijiji vinavyozizunguka hifadhi zake ikiwemo ya Mkomazi.