Aliyekuwa Kiongozi wa Walinzi wa Chama cha Wananchi (CUF) Zanzibar, Thiney Juma Mohamed amemshauri Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sheriff Hamad kuacha kufukuza viongozi wa CUF huku akimsihi kufanya mazungumzo na Profesa Ibrahim Lipumba ili kuuondoa mgogoro wa kikatiba ulioko katika chama hicho ambapo inadaiwa wawili hao ndio mzizi wa mgogoro huo.
Mohamed amesema kuwa, licha ya mgogoro huo kufikishwa mahakamani, maamuzi ya kisheria yatakayo tolewa hayatasaidia kuutatua mgogoro huo.
“Kitendo cha Maalim Seif kugoma kufanya mazungumzo na Lipumba kinazidi kukipasua chama, na wala maamuzi ya mahakama hayatatatua mgogoro sababu akishinda maalim ugomvi uko palepale na akishinda Lipumba pia utabaki vilevile,” amesema na kuongeza.
“Leo hii Seif kajikita Zanzibar na Lipumba Bara, hiki chama ni cha kitaifa kikijipasua hatutafikia lengo la kuongoza dola. Namuomba Seif kwa kuwa mgogoro huu uko kiganjani kwake aukunjue moyo ili uishe.”
Kuhusu kufukuzwa uanachama, Mohamed amedai kitendo hicho kilikuwa kinyume cha katiba ya CUF kwa kuwa inaelekeza kuundwa kwa Kamati ya nidhamu na Maadili ya Tawi ili kuchunguza mwanachama mwenye makosa na kwamba haikuundwa kamati hiyo pia hakuna uchunguzi wowote uliofanywa dhidi yake na kudai kuwa uongozi wa tawi lake ulipewa Maelekezo ya kumfukuza na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif bila ya kufuata utaratibu.
“Mimi ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa na Nilichaguliwa na Mkutano Mkuu wa Wilaya. Hivyo, kwa Mjibu wa Katiba ya CUF ya mwaka 1992 Toleo la 2014, Ibara ya 10 (5) nainukuu: Mwanachama yeyote amabaye ana wadhifa katika chama au Serikali (kiongozi kwa tiketi ya Chama) anaweza kuachishwa au kufukuzwa uanachama na Baraza Kuu la uongozi la Taifa au Mkutano Mkuu wa Taifa kwa mujibu wa Masharti ya Katiba hii,” amesema na kuongeza.
“Kwa hiyo, Tawi halina uwezo wa kumfukuza uanachama Kiongozi wa Chama katika ngazi ya Taifa kwa kuzingatia kuwa Mimi ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa.”
Kuhusu kutowa Taarifa kwa Vyombo vya Habari pasipo kuwa msemaji wa Chama amesema “Nasikitika kusema kwamba sijawahi hata siku moja kutowa Taarifa kwa vyombo vya habari kama Msemaji wa Chama Bali niliwahi kutowa Maoni yangu Binafsi Katika Gazeti la Jamboleo la Tarehe 26/11/2016 siku ya Jumamosi ambayo yalinukiliwa na mWandishi kwa kichwa cha habari Kamandawa CUF amshukia Maalim Seif.”
