Profesa Ibrahim Lipumba, anayetambulika na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kushikilia nyadhifa ya Uenyekiti wa Chama cha Wananchi(CUF) licha ya baadhi ya viongozi wa chama hicho kudai wamemfuta uanachama, amesema CUF imepokea kwa huzuni kubwa taarifa ya kifo cha Spika Mstaafu Samuel Sitta kilichotokea nchini Ujerumani alikoenda kupata matibabu.
Lipumba amesema kuwa, “Kwa niaba ya CUF na kwa niaba yangu binafsi tunatoa salamu za rambi rambi kwa Mke wa Marehemu, Mama Magreth Sitta, familia yake na ukoo wote wa Mtemi Fundikira wa Unyanyembe kwa msiba huu mkubwa.
Marehemu Samuel Sitta ametoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi yetu kama Mbunge wa jimbo la Urambo, mkoa wa Tabora, Waziri wa Serikali ya Muungano toka awamu ya Mwalimu Nyerere, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Spika wa Bunge Maalum la Katiba.”
Lipumba amesena mchango wa marehemu Sitta katika ujenzi wa demokrasia ulidhihirika pale alipokuwa Spika wa Bunge la Muungano mwaka 2005 – 2010. Kutokana kwamba katika kipindi chake kama Spika, Bunge liliimarika kama chombo cha kuiwajibisha serikali.
“Chini ya uongozi wake Kamati ya Bunge iliweza kufanya uchunguzi wa kina kuhusu kashfa ya ufisadi wa ufuaji umeme wa kampuni ya Richmond. Kama Spika aliwatendea haki Wabunge wa vyama vya upinzani nakuwapa fursa yakuihoji na kuiwajibisha serikali.
Taifa la Tanzania limempoteza kiongozi mashughuli katika kupambana na ufisadi na kujenga demokrasia ndani ya nchi yetu. Mchango wake wa kuimarisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utaendelea kukumbukwa daima.” amesema.
Ameongeza kuwa “Tunamuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.”