Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Dar es salaam kimekanusha vikali juu ya kuwepo kwa njama zinazodaiwa kutumiwa na wajumbe wa chama hicho katika Uchaguzi wa Meya wa Manispaa ya Kinondoni uliofanyika jana ambapo CCM ilishinda kiti hicho cha Umeya.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar Es Salaam Ramadhan Madabida amesema kuwa Uchaguzi wa Umeya Manispaa ya Kinondoni ulikuwa wa huru na haki na ulifuata taratibu zote kwa mujibu wa Sheria.
Aidha Mwenyekiti huyo amesema kuwa Wajumbe 18 wa CCM walishiriki katika mchakato wa upigaji kura baada ya Wajumbe wa upinzani kutoka nje ya ukumbi na kususia mchakato huo wa upigaji kura baada ya kudai kuwepo njama na hujumaza katika mchakato huo.
Mwenyekiti Madabida amewataka viongozi na wanachama wa vyama vya upinzani nchini kuacha kufanya siasa za kichochezi na vurugu ambazo hazina mlengo wowote katika kuendeleza nchi badala yake wajikite katika kufanya mambo yatakayojenga amani ya nchi sambamba na kuhamisha umma kuhusu swala zima la maendeleo.