Na Asukile Mwalwembe, MAKETE
Vipodozi vyenye thamani ya shilingi milioni moja na nusu vimeteketezwa kwa moto baada ya mfanyabiashara mmoja kusalimisha bidhaa hizo zilizokwisha muda wake wa matumizi lakini bado alikuwa akiendelea kuziuza.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuteketezwa kwa vipodozi hivyo kaimu mganga mkuu wa wilaya ya Makete mkoani Njombe Bw, Boniface Sanga amesema kuwa kitendo alichofanya mfanyabiashara huyo ambaye jina lake limehifadhiwa ni mfano wa kuigwa kwa taifa na jamii kwa ujumla.
Bw. Sanga amewaomba wafanya biashara kusoma muda wa kuisha matumizi ya bidhaa pamoja na wanunuzi kuzingatia elimu inayo tolewa ya kuisha muda wa matumizi kwa kila bidhaa.
Aidha kaimu mganga mkuu huyo amesema kuwa wananchi wanaweza kupata madhara mbalimbali ikiwemo ugonjwa wa saratani mara baada ya kutumia bidhaa zilizoisha matumizi ya muda wake.
Kwa upande wake mmoja wa mashuhuda aliye shuhudia wakati vipodozi hivyo vinateketezwa Bw. Christopher Msika ametoa wito kwa wananchi kuhakikisha wananunua vipodozi vilivyo thibitishwa na mamlaka ya chakula na dawa TFDA ili kuepusha kutokea kwa madhara mbalimbali.
