Ofisa Jiolojia Mwandamizi katika Wakala wa Jiolojia Tanzania, Gabrel Mbogoni amesema hadi sasa hakuna teknolojia ya kubaini tetemeko la ardhi kabla halijatokea, hivyo kinachotakiwa ni wananchi kukaa tayari wakati wote.
Mbogoni amesema hayo kufuatia tetemeko la ardhi lilillotokea mkoani Kagera jana na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 10 na wengine kujeruhiwa.
Tetemeko hilo la kipimo cha 5.7 ritcher ni la pili baada ya lile lililotokea katika eneo la Oldoinyo Lengai mkoani Arusha mwaka 2007 likiwa na ukubwa wa 5.9 ritcher.
Mbogoni amesema ukubwa wa madhara wa tetemeko unategemea eneo linakopita, kina cha mawimbi kutoka usawa wa ardhi, ugumu wa miamba iliyopo na aina ya nyumba au miundombinu iliyopo.
Amesema kuwa tetemeko lililotokea Oldoinyo Lengai licha ya kusababisha mpasuko wa mita nne kwenye ardhi, halikuleta athari kubwa kwa binadamu kutokana na aina ya nyumba za miti wanazojenga wenyeji, ambazo huhimili mtikisiko.
Ili kujiokoa, Mbogoni amesema wananchi wachukue tahadhari kwa sababu mara nyingi tetemeko moja linapotokea yanatokea mengine yanayoweza kuwa na ukubwa unaokaribiana na ule wa mwanzo.
Amewataka wananchi kutokimbia ovyo wanaposikia matetemeko ya ardhi, bali wabaki wakiwa wametulia mahali palipo na usalama.
“Kwa mfano, kama uko ndani unaweza ukajificha kwenye uvungu wa meza au kitanda au ukasimama katika makutano ya kuta.
“Baada ya mtikisiko unatakiwa kutoka nje na kukaa mahali ‘peupe’,” amesema.
Amewaonya watu kutokaa karibu na vitu virefu kama majengo, nguzo za umeme au miti kwa sababu chochote kinachoweza kuanguka.
Amesema endapo mtu ataangukiwa na vitu vizito, asitumie nguvu nyingi kujinasua wala kupiga kelele mfululizo, kwa kuwa anaweza kuishiwa nguvu kabla hajaokolewa.
