Wadaiwa kuua na kufukia mwili chooni

POLISI mkoani Kilimanjaro inawashikilia watuhumiwa watano kwa tuhuma za kumuua kwa kukusudia mwanamke Neema Ndewera (65), kwa kumchoma kisu shingoni na sikio la kulia.

Akitoa taarifa hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Willbrod Mutafungwa, watuhumiwa hao walifanya tukio hilo la kinyama Julai 10, mwaka huu ambapo baada ya tukio hilo walifukia mwili wa marehemu kwenye shimo la choo cha nje ya nyumba yake.

Alisema Ndewera alikuwa akiishi peke yake katika kata ya Mbokomu, ambako Juni mwaka huu aliaga anasafiri kwenda Arusha kuwaona watoto wake, ambapo alimuomba jirani yake Michael John kuwa mwangalizi wa mifugo yake ambayo ni mbuzi wawili, ng’ombe mmoja na kuku.

Alisema mwanzoni mwa Julai, alirudi nyumbani kwake na kukuta mbuzi na kuku wameuzwa, hali iliyomlazimu kumuuliza John kuhusu suala hilo ambalo hakupewa majibu ya kuridhisha. 

Mutafungwa alisema kutokana na hali hiyo Julai 10, John akishirikiana na watuhumiwa wenzake, wote kwa pamoja walimuua Ndewera ili asiwashtaki kwa wizi wa mifugo.

Alisema baada ya tukio hilo watuhumiwa hao waliuza ng’ombe aliyebaki kwa Sh 400,000 kisha kugawana fedha, ambapo walidanganya kuwa Ndewera anaumwa na amesafiri kwenda Dar es Salaam kwa mtoto wake kwa matibabu.

Alisema Agosti 12, Polisi ilipata taarifa hizo kutoka kwa raia wema, ambapo walifika eneo la tukio na kuukuta mwili wa marehemu ukiwa umefunikwa kwenye shimo la choo ukiwa na kisu shingoni, ambapo uchunguzi ulifanywa na madaktari na kukabidhiwa kwa ndugu wa marehemu.

Kamanda aliwataja watuhumiwa wa tukio hilo ni John (24) fundi ujenzi, Nevance Reginald (46), Mussa Issa (23), Fausta Naftari (29) na Magreth John (53), wote wanne wakijishughulisha na kilimo.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo