Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb) akitoa taarifa kwa Vyombo vya
Habari kuhusu zoezi la kuondoa watumishi
hewa katika orodha ya malipo ya mishahara serikalini ofisini kwake mapema leo.
Baadhi
ya waandishi wa habari wakimsikiliza Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.
Angellah J. Kairuki (Mb) alipozungumza leo ofisini kwake jijini Dar es
Salaam.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Mhe. Angellah
J. Kairuki (Mb) akifafanua jambo kwa
waandishi wa habari (hawako pichani) kuhusu utekelezaji wa agizo la kuondoa
watumishi hewa katika orodha ya malipo ya mishahara Serikalini ofisini kwake
mapema leo.
Kama
mnavyokumbuka, mnamo tarehe 15 Machi, 2016 Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwaagiza Wakuu wa Mikoa na Waajiri wote
kwa ujumla kuchukua hatua ya kuhakikisha katika Mikoa au Taasisi zao hakuna
watumishi hewa ifikapo tarehe 30 Machi,
2016.
Katika
kutekeleza agizo hilo la Mheshimiwa Rais, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya
Utumishi wa Umma na Utawala Bora imekuwa ikifuatilia utekelezaji wa agizo hili
na mnamo tarehe 26 Mei, 2016 waajiri
wote waliagizwa kuwasilisha taarifa za mwisho za zoezi la kuwabaini na
kuwaondoa watumishi hewa katika orodha za malipo ya mshahara (payroll) ifikapo
mwisho wa Mwezi Juni, 2016. Waajiri wote walielekezwa kutuma taarifa tajwa kwa
kuzingatia muundo wa uandaaji na uwasilishaji wa taarifa hizo kwa kuainisha
mambo yafuatayo:-
·
Jina la Taasisi;
·
Fungu (Vote);
·
Cheki Namba ya Mtumishi;
·
Jina Kamili la Mtumishi;
·
Cheo cha Mtumishi;
·
Jina la Tawi la Benki ambalo
mshahara wa mtumishi umekuwa ukipitishwa/ukilipwa;
·
Akaunti Namba ya Benki ya
Mtumishi;
·
Tarehe ambayo Mtumishi
aliondolewa kwenye Mfumo wa Taarifa ya Kiutumishi na Mshahara;
·
Kiasi cha fedha zilizolipwa
kwa mtumishi husika tangu alipotakiwa kuondolewa hadi tarehe aliyoondolewa
kwenye Mfumo;
·
Sababu ya kuondolewa kama
utoro, kufariki dunia, kuacha kazi, kustaafu n.k.
·
Hatua zilizochukuliwa na
mwajiri dhidi ya watumishi hwa waliobainika kama kurejesha fedha, na Maafisa
wengine wa Taasisi husika waliosababisha uwepo wa Watumishi Hewa kuwachukulia
wahusika hatua za kinidhamu/kisheria.
Aidha,
waajiri 264 kati ya waajiri wote 409 wamewasilisha taarifa zao kuhusu uwepo wa
watumishi hewa. Kati ya waajiri 264 waliowasilisha taarifa zao, waajiri 63
wamethibitisha kwamba hawana watumishi hewa katika Taasisi zao na waajiri 201
wana watumishi hewa mmoja (1) na kuendelea.
Katika
kufanikisha zoezi hili Ofisi yangu imechukua hatua kadhaa ikiwemo kuendelea
kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa Maafisa Utumishi wenye dhamana ya kutumia
Mfumo wa Malipo ya Mshahara, kukuza uwajibikaji kwa Maafisa wanaosimamia malipo
ya mishahara kwa kuwachukulia hatua za kinidhamu/kisheria wanaobainika kusababisha
watumishi hewa, kufanya uhakiki wa kushtukiza na kuanza safari ya kuunganisha
Mfumo wa Malipo ya Mishahara na mifumo mingine mikubwa kama ya NIDA, RITA na
Baraza la Mitihani la Taifa, na kuwezesha mfumo kuwaondoa moja kwa moja
(automatically) watumishi waliofikisha umri wa kustaafu kwa lazima.
Pamoja
na taarifa hiyo, zipo Taasisi 145 ambazo hazijawasilisha taarifa iwapo wana
watumishi hewa au hawana watumishi hewa. Waajiri ambao hawajawasilisha taarifa
zao wamegawanyika katika makundi yafuatayo:-
·
Mabaraza mbalimbali 11
·
Bodi mbalimbali 10
·
Vyuo Vikuu 25
·
Hospitali 3
·
Ofisi za Makatibu Tawala wa
Mikoa 12
·
Mamlaka mbalimbali 6
·
Tume mbalimbali 10
·
Mamlaka za Serikali za Mitaa
38
·
Taasisi za Umma na Wakala 30
Aidha,
kuanzia tarehe 15 Agosti, 2016 Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma
na Utawala Bora inaendesha zoezi la uhakiki wa kushtukiza katika Taasisi sabini
(70) za Serikali zikiwepo Wizara, Idara za Serikali Zinazojitegemea,
Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi za Umma kwa
madhumuni ya kujiridhisha kwamba taarifa za watumishi hewa zilizowasilishwa na
waajiri ni sahihi.
Vilevile,
napenda kuwataarifu pia kwamba taarifa kamili ya watumishi hewa itatolewa baada
ya kupata taarifa hizo kutoka kwa waajiri ambao hawajawasilisha taarifa hizo na
kukamilika kwa zoezi la uhakiki wa Taasisi sabini (70) linaloendelea sasa.
Naagiza Taasisi zote hazijawasilisha Taarifa za Watumishi Hewa kufanya hivyo
kabla au ifikapo tarehe 26 Agosti, 2016.
Ofisi hii itawasilisha taarifa rasmi ya
watumishi hewa kwa Mheshimiwa Rais ikiwa na orodha na majina ya Taasisi ambazo
zimewasilisha taarifa ya watumishi hewa na na zile ambazo hazijawasilisha
taarifa hizo.
Taarifa hizo ziwasilishwe kwa kuzingatia mfumo
uliotolewa katika barua ya tarehe 26
Mei, 2016 kwa nakala ngumu na nakala laini (Soft Copy/Hard Copy) kupitia
anuani ya barua pepe ps@utumishi.go.tz.
Na kwa nakala ngumu iwasilishwe Ofisi ya Katibu Mkuu (Utumishi).
Imetolewa
na Mhe. Angellah J. Kairuki (MB.) WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS MENEJIMENTI YA
UTUMISHI WA UMMA
NA UTAWALA BORA,
20
AGOSTI, 2016