Wanafunzi 80 wa shule ya sekondari ya Aldersgate inayomilikiwa na Kanisa la Mungu iliyopo katika Halmashauri ya
mji wa Babati mkoani Manyara wamenusurika kuteketea kwa moto baada ya moto kuzuka na kuteketeza bweni,samani na vitu mbalimbali mali ya wanafunzi hao,ikiwa ni siku moja kabla ya uongozi wa shule hiyo kuifunga kwenda likizo ya
muda mfupi.
Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wakizungumzia tukio hilo lililozusha taharuki iliyochangia wanafunzi wawili
kupoteza fahamu na kulazwa katika hospitali ya Mrara ya Malmashauri ya mji wamedai hawatambui chanzo cha moto
huo kuteketeza mali zao,lakini pia wakilaumu kuchelewa kwa askari wa jeshi la zimamoto huku mkuu wa shule hiyo Bw
Dillo Fredson akidai chanzo cha moto huo ni hitilafu ya umeme.
Nae Kamanda wa Jeshi la zimamoto mkoani Manyara Bw Heriel Kimaro amesema licha ya kutumia lita 12,000 kuzima
moto huo kwenye bweni hilo lenye vyumba vitano amedai kushangazwa uongozi wa shule hiyo kuchelewa kutoa taarifa
mapema kwa kupiga simu na.114 waliyokuwa wameitoa kwa uongozi huo.
Hata hivyo Kamanda wa Polisi mkoani Manyara Afande Francis Jacob amethibitisha kutokea kwa tukio hilo usiku lakini
amedai watalazimika kuwahoji mlinzi na mlezi ili kujiridhisha na endapo itabainika kuzembea watafikishwa kizimbani
kwani majeshi yote mawili zimamoto na polisi walishatoa elimu na maelekezo ya majanga ya moto.