Ngariba huyo, Mkazi wa Kijiji
Rung’abure, Christina Mairo (55) maarufu kwa jina la Wansato alifikia
uamuzi huo baada ya kuhubiriwa na wachungaji wa Kanisa la Jeshi la
Wokovu waliomtembelea nyumbani kwake kumweleza madhara ya kukeketa
watoto wa kike.
Pamoja na ‘kuokoka’ na kutangaza
kuachana na shughuli hiyo, ngariba huyo pia aliteketeza mkoba wake wenye
zana za ukeketaji baada ya kuingiwa na somo la ubaya na madhara ya
ukeketaji.
Akizungumza baada ya kutangaza kuacha
kazi hiyo na kuchoma moto zana za ukeketaji, Ngariba huyo alikiri
kushuhudia mateso wanayopata wanawake walikeketwa wakati wa kujifungua
watoto.
Mairo amesema ameamua kuachana na kazi
hiyo ambayo inamfanya kuandamwa baada ya kujua matatizo yanayowakumba
wajawazito wakati wa kujifungua.
Mratibu wa mradi wa kutokomeza vitendo
vya ukatili wa kijinsia Kupitia Jumuiya ya Kikristo Tanzanja (CCT),
Sophia Mchonvu alisema kwa kipindi cha miaka 10, shirika hilo na
wanaharakati wamekuwa wakimtembelea ngariba huyo kumshawishi kuachana na
kazi hiyo bila mafanikio.
“Tukio la ni matunda ya harakati
zilizoanza miaka 10 iliyopita. Hii ni ishara njema katika mapambano
dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia wilayani Serengeti na maeneo
mengine ambako vitendo vya ukeketaji vinafanyika,” alisema Mchonvu .
Mchungaji wa kanisa hilo, Wilson Mwile
alisema vita dhidi ya ukatili vinakwamishwa na imani, mila na desturi
kandamizi dhidi ya wanawake.
Diwani wa Kata ya Rung’abure, Elias Mirengo aliwataka ngariba wengine kuacha shughuli hiyo.
Mmoja wa watoto wa ngariba huyo, Rachel
Thomas aliwashukuru waliofanikisha mama yake kuachana na kazi hiyo ya
ukeketaji watoto wa kike.
CHANZO: Mwananchi