Mwanafunzi wa kidato cha nne Butinzya sekondari Wilaya ya Bukombe Mkoa wa
Geita amenusurika kupoteza maisha wakati akijaribu kutoa mimba aliyodai alipewa na
mwalimu wake.
Akizungumza akiwa amelazwa katika zahanati ya Msonga iliyopo mjini Ushiromba leo
mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 17 alimtaja mhusika kuwa ni mwalimu wake
aliyeanza mahusiano naye tangu mwaka 2015 na kuwa anampatia zawadi ndogondogo na
fedha Sh 10,000 hadi 15,000 za kujikimu.
“Nilibeba ujauzito mwezi Juni mwaka huu, nilipomwelezea ndipo akaamua kunipeleka
hospitalini hapo kutolewa, lakini ilipofika saa 3:00 usiku tumbo lilianza kuniuma huku damu
zikinitoka kwa wingi niliamua kumweleza rafiki yangu ninayekaa naye akaaite walimu waje
kunisaidia ndipo waliponileta hospitalini hapa,”alisema
Mganga mfawidhi wa zahanati ya Msonga kitengo cha wazazi wazazi, Dk Makopudo Hergard
alisema mwanafunzi huyo alipokelewa majira ya saa 7:30 usiku akiwa na hali mbaya huku
akitokwa na damu nyingi baada ya kutoa mimba.
Dk Hergard alisema baada ya kumuhoji tuligudua mwanafunzi huyo alitoa mimba lakini
mimba haikutoka yote hivyo walimwekea dripu tano za maji na kumchoma sindano ya kukata
damu hali na hivi sasa hali yake inaendelea vizuri lakini amepewa rufaa kwenda hospitali ya
Wilaya kwa ajili ya uchuguzi zaidi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo alisema taarifa za mwanafunzi
huyo kunusurika kifo anazo na kwamba taratibu zilizopo ni kumtafuta mwalimu
anayehusishwa na kitendo hicho na atakapokamatwa hatua za kisheria dhidi yake zitafuata.
