MAHAKAMA
Kuu Kitengo cha Biashara imeamuru Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya
IPP, Reginald Mengi afike mahakamani kujieleza kwa nini asifungwe
gerezani kwa kushindwa kutekeleza hukumu inayohusu malipo ya Sh bilioni
1.2.
Mengi
anatakiwa kufika mahakamani hapo Agosti 24, mwaka huu kujieleza
kutokana na kushindwa kutekeleza hukumu iliyomtaka kuwalipa
wafanyabiashara watatu, Muganyizi Lutagwaba, Eric Mshauri na Charles
Mgweo, Sh bilioni 1.2.
Alitakiwa
kuwalipa fedha hizo kutokana na mgogoro wa malipo ya uuzwaji wa hisa
katika Kampuni ya Douglas Lake Minerals Ltd ambayo kwa sasa inaitwa
Handeni Gold Inc.
Kwa
mujibu wa hati ya wito wa kufika mahakamani, Mengi anatakiwa kufika
mahakamani hapo Agosti 24, mwaka huu ili ajieleze kwa nini asifungwe
gerezani kama mfungwa wa madai kama sehemu ya kukazia hukumu hiyo.
Mahakama
imetoa hati hiyo kutokana na wafanyabiashara hao kuwasilisha maombi
katika hatua ya kukazia hukumu iliyotolewa Januari 28, mwaka huu na Jaji
Agathon Nchimbi wa mahakama hiyo.
Katika
hati ya kiapo ya wafanyabiashara hao, inadaiwa walifungua kesi dhidi ya
Mengi na Kampuni ya K.M. Prospecting Limited, wakidai malipo yaliyokuwa
yamebakia ya dola 428,750, 100,000 na 70,000, kwa kila mmoja.