Watuhumiwa 10 wakiwemo raia wawili wa Guinea, wamefikishwa katika
mahakama ya hakimu mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka
ya kujihusisha na mtandao wa uhalifu na kukutwa na meno ya Tembo yenye
thamani ya sh bilioni 4.6.
Washitakiwa hao wamesomewa mashitaka matatu chini ya sheria ya uhujumu
uchumi na sheria ya uhifadhi wa wanyamapori ambapo walisomewa na jopo la
mawakili wanne wa serikali, wakiongozwa na Paul Kadushi, mbele ya hakimu
mkazi mkuu, Dk Yohana Yongolo.
Katika mashitaka yao inadaiwa kuwa tarehe tofauti kati ya Aprili 6 na
Juni 26, mwaka huu Dar es Salaam, kwa pamoja wanadaiwa kupanga,
kuratibu, kusimamia na kufadhili mtandao wa uhalifu kwa kuuza, kupokea
na kusafirisha nyara za serikali ambazo ni vipande 660 vya meno ya Tembo
bila kuwa na kibali kutoka kwa mkurugenzi wa wanyamapori.
Hakimu Yongolo amesema washitakiwa hawatakiwi kujibu mashitaka kwa kuwa
mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo isipokuwa mahakama
kuu, ambapo upande wa jamhuri umedai upelelezi wa kesi hiyo bado
haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Kabla kesi hiyo hajahahirishwa mshitakiwa Victor alidai anaumwa
kwasababu ya kupigwa wakati akiwa kwenye kituo cha polisi, hivyo
aliiomba mahakama itoe maelekezo ili apewe matibabu hali iliyomlazimu
hakimu Yongolo aliamuru mshitakiwa huyo apewe matatibu akiwa gerezani.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai 28, mwaka huu na washitakiwa
wamerudishwa rumande kwa kuwa mashitaka yanayowakabili hayana dhamana.
CHANZO: ITV