Kutokana
na kuonekana kushindwa kutoa magazeti katika kipindi cha miaka mitatu,
serikali imetangaza rasmi kuyafutia usajili magazeti 473 kutokana na
kushindwa kutoa nakala katika kipindi cha miaka hiyo mitatu.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,
Mh. Nape Nnauye amesema kuwa wamiliki wa magazeti hayo wamevunja
sheria na kwa mujibu wa kifungu 23(1) cha Sheria ya Magazeti ambacho
kinampa mamlaka ya kuyafutia usajili, anayafungia magazeti hayo.
“Kuna
magazeti yana miaka mitatu sasa bado hayajatolewa nakala mengine
yalikuwa yanatoa na baadae yakaacha na mengine hayajatoa kabisa, haya
yote natangaza kuanzia leo yamefutwa usajili wake,” alisema Waziri Nape.
Waziri
Nape alisema kuanzia sasa hairuhusiwi kwa mtu yoyote kuchapisha nakala
za magazeti yaliyofungiwa na kwa kufanya hivyo atakuwa amekiuka Sheria
ya Magazeti sura ya 229, kifungu cha 6 na hivyo atachukuliwa hatua kwa
mujibu wa sheria.
Aidha
Waziri Nape aliongeza kuwa kama kuna mmiliki wa magazeti ambayo
yamefungiwa angependa kuendelea kuchapisha nakala za gazeti lake,
milango ipo wazi kuwasilisha maombi mapya ya usajili kwa kufuata sheria
zilizopo.
