Shughuli za kimaendeleo katika kijiji cha Utweve kata ya Ukwama wilayani
Makete mkoani Njombe kuanzia jana zimesimama Kwa muda usiojulikana huku
wananchi wa kijiji hicho wakihitaji hatma ya watuhumiwa wa mauaji ya mtoto
mmoja wa kijiji hicho
Hayo yamekuja kutokana na kuanza kujadili Ajenda za mkutano juu ya ujenzi
wa Zahanati kijijini hapo ndipo wananchi hao wakapinga kujadili Ajenda hiyo
badala yake wakataka wapate mrejesho wa kinachoendelea juu ya watuhumiwa wa
mauaji waliowekewa dhamana kama wamekamatwa ama lah kufuatia maazimio
waliyowekeana kwenye mkutano uliofanyika Juni 22 mwaka huu.
Wananchi hao wamesema hawapo tayari kufanya shughuli zozote za maendeleo
mpaka wapate hatma ya suala hilo
Pia wameweka wazi kuwa katika mkutano uliopita uliofanyika kijijini hapo
Juni 22 mwaka huu ulimalizika salama na haukuwa na vurugu yeyote kama
inavyodaiwa kuwa wapo wananchi waliofanya vurugu
Baada ya majadiliano ya muda mrefu wananchi hao wameazimia kuwa wanahitaji
mkuu wa wilaya ya Makete afike kijijini hapo na viongozi wengine wa wilaya ili
wasikilize kilio chao.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kijiji hicho Bw Rauteli Sanga amewaomba
wananchi pamoja na wafiwa kuwa na uvumilivu wakati wananendelea na ufuatiliaji
wa suala hilo la mauaji wakati vyombo vya dola vikilishughulikia kwa upande
wao.