Siku maiti ya Brain ilipozikwa kimakosa.
Na Joseph Ngilisho, UWAZI
ARUSHA: Katika hali isiyokuwa ya
kawaida, wimbo la miili ya marehemu kuchanganyiwa ndugu linazidi
kutikisa nchi baada ya mwili wa mtoto Brian Kamnde (1/6) uliokuwa
umezikwa kwa saa 24, kulazimika kufukuliwa kufuatia kubainika kuwa, siyo
uliyokusudiwa na kwamba, ulikuwa ni wa mtoto Valentino Alfa Makundi
(0/4)
ENEO LA TUKIO
Tukio la kufukuliwa kwa mwili huo,
lilijiri Mtaa wa Lorovono, Kata ya Sokoni jijini hapa mwishoni mwa wiki
iliyopita baada ya kubainika kuwa, mwili huo ulitolewa kimakosa katika
Chumba cha Kuhifadhia Maiti (mochwari) kwenye Hospitali ya Mkoa, Mount
Meru.
NDUGU WA MAITI YA PILI WABAINI
Mkanganyiko wa tukio hilo ulitokana na
ndugu wa marehemu Brian aliyefukuliwa Mtaa wa Lorovono kufika mochwari
kwa lengo la kumchukua mpendwa wao huyo na kupigwa butwaa baada ya
kutafutwa kwa marehemu huyo bila mafanikio.
MAELEZO YA MAMA MZAZI
Mama mzazi wa Brian, Neserian Elisha,
mkazi wa Nambere jijini hapa, alisema kuwa baada ya kufika mochwari
kuchukuwa mwili wa mtoto wake hawakuuona na kuoneshwa mwili wa
Valentino.
Ndugu wakifukua maiti.
SITOFAHAMU YAIBUKA
Hali hiyo ilizua sintofahamu kwa upande
wa wanandugu hao, ndipo uongozi wa mochwari hiyo walipolazimika
kufuatilia na kubaini kwamba, mwili wa Brian ulitolewa kimakosa na
kuwataka ndugu waliouzika eneo la Sokoni kufika mochwari hapo haraka ili
kuutambua mwili wao sahihi. Wakati huo tayari mwili wa Brian ulikuwa
umeshazikwa jana yake.
LAWAMA ZA MHUDUMU WA MOCHWARI
Francis Coster ni mmoja wa wahudumu wa
chumba cha maiti, yeye alisema tukio hilo lilisababishwa na wanandugu
kutokuwa makini wakati wa kuchukua mwili wa marehemu wao.
Jeneza likitolewa kaburini.
BABA MDOGO WA MAREHEMU
Kwa upande wake, baba mdogo wa marehemu,
Valentino, Godson Makundi alisema wamesikitishwa sana na tukio hilo na
kuongeza kuwa ni la aibu kwa hospitali.
“Sisi baada ya kufika katika chumba cha
maiti tulikuta umati wa wananchi ambao walikwenda kuchukua miili ya
ndugu zao waliopata ajali iliyotokea hapa Arusha, hivyo hatukuruhusiwa
kuingia, bali walitutaka kuonesha karatasi yenye utambuzi wa marehemu na
kutolewa akiwa ameshaoshwa na kusitiriwa kwenye jeneza. Tukaenda
kuzika, kesho yake tukashangaa kuambiwa tulizika mwili ambao haukuwa wa
mwanetu,” alisema Makundi.
Mama wa Valentino akithibitisha kuwa si mwanaye aliyezikwa.
MAMA MZAZI AZIMIA
Wakati wa kulifukua jeneza lenye mwili
wa Brian ambapo usahihi lilitakuwa kuwa na mwili wa Valentino, mama wa
Valentino alipoteza fahamu baada ya kujiridhisha kuwa, mwili huo haukuwa
wa mwanaye.
Mama Valentino akibebwa baada ya kuzirai.
MIILI YAENDA KUZIKWA
Mwili wa marehemu Brian ulipelekwa
kuzikwa tena eneo la Mbokomu wilayani Moshi Mkoa wa Kilimanjaro huku
mwili wa Valentino ukienda kuzikwa kwenye kaburi lilelile lilofukuliwa
Mtaa wa Lorovono.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Arusha, ACP Charles Mkumbo alithibitisha kutokea kwa tukio na kusema
wao ndiyo waliotoa kibali cha kufukuliwa kwa mwili huo ili ukazikwe eneo
lililostahili.
GUMZO KUBWA, MUHIMBILI YATAJWA
Tukio hilo limezua gumzo kubwa na kuacha
waombolezaji vinywa wazi ambapo baadhi ya wananchi wa Jiji la Arusha
wamesema ni la aibu na la aina yake huku wengine wakikumbushia matukio
mawili ya miili kubadilishwa kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar.
Hospitali ya Taifa Muhimbili iliwahi
kuingia kwenye mkasa kama wa Arusha mara mbili baada ya Aprili mwaka
huu, kutoa mwili wa marehemu kwa watu tofauti ambao nao bila ya kujua,
waliusafirisha na kuuzika Usangi, Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Mwili wa Janeth Bambalawe (65) wa Gongo
la Mboto uliozikwa Usangi ulirejeshwa Dar ili ukabidhiwe kwa wahusika
ambapo ulichanganywa na mwili wa Amina Msangi (79) uliostahili kuzikwa
Usangi.
Pia, Juni mwaka huu, Muhimbili ilirudia
kosa hilo kwa kuruhusu mwili wa marehemu kuchukuliwa na ndugu
wasiohusika na hivyo kuleta mtafaruku mkubwa ambapo mwili wa mwanafunzi
aliyekuwa kidato cha tatu, Shule ya Sekondari Ulongoni, Dar, Mamy
Venancy ulienda kuzikwa Mtwara kwa kuuchanganya na wa marehemu
aliyetajwa kwa jina moja la Theresia, mwenyeji wa Mtwara.
Chanzo: http://globalpublishers.co.tz/
