Magufuli Amteua Kinana Kuwa Katibu Mkuu CCM Licha ya Kuomba Kujiuzulu

KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ameandika barua ya kujiuzulu nafasi hiyo kwa Mwenyekiti mpya wa CCM, Rais John Magufuli, lakini Rais amekataa barua yake hiyo.

Badala yake, Rais Magufuli amemtaka Kinana na manaibu katibu wakuu wawili na sekretarieti nzima ya chama hicho, kuendelea na kazi. 

Hayo yalisemwa na Rais Magufuli wakati akitoa hotuba ya kushukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu Malumu wa CCM, mjini hapa.

“Nimepata barua ya Kinana ya kujiuzulu nafasi yake pamoja na wakuu wa idara za sekretarieti. Nimeamua Kinana na sekretarieti yote waendelee kuwepo. 

“Kama kutakuwa na haja baadaye nitaitisha kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na siyo leo,” alisema Magufuli, akiwatangazia wajumbe hao wa kikao cha Mkutano Mkuu, ambacho ni kikao cha juu cha chama.

Alisema kwa kuwa mkutano huo ndiyo wenye uamuzi wa mwisho kuhusu masuala ya chama, hivyo anawauliza wajumbe kama wamekubaliana na pendekezo lake hilo la Sekretarieti ya chama iendelee.

“Nawauliza wajumbe mnaafiki?” Ambapo wote kwa kauli moja walisema; “Ndiyo.” Magufuli alisema kulikuwa na watu waliokuwa wamejipanga kuchukua nafasi hizo za sekretarieti, lakini “sasa imekula kwao”. Hakutaja watu hao.

Akiongeza kuwa; “Nitaendelea kuwa na Kinana na nina imani yeye na sekretarieti nzima watasimamia vizuri mambo kadhaa niliyoagiza yasimamiwe haraka.”

Magufuli alisema CCM ni chama cha aina yake duniani, kwa kuwa kila upande kuna fursa ya ushauri kutoka kwa wazee wastaafu (huku akiwataja kwa majina), jambo linalofanya kazi iliyo mbele yake kuwa nyepesi.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo