Na Mwene Said, Globu ya Jamii.
Upande
wa utetezi, katika rufani ya kesi inayomkabili Kamishna wa zamani wa
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake
wanaokabiliwa na mashtaka ya kujipatia Dola za Marekani million sita,
leo uliomba kuahirisha kusikilizwa rufani hiyo baada ya mawakili wawili
kuwa na udhuru ikiwamo ugonjwa.
Dk.
Masumbuko Lamwai alitoa maombi hayo leo mbele ya Jaji Edson Mkasimongwa
aliyepangiwa kusikilizwa rufani ya kuondolewa shtaka la kutakatisha
fedha pamoja na maombi ya dhamana ya washtakiwa hao katika Mahakama Kuu
Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Dk.
Lamwai alisema kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa rufani ya Jamhuri
kupinga kuondolewa shtaka la kutakatisha fedha lakini Wakili Majura
Magafu alikuwa na kesi nyingine katika Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha.
Pia, alidai kuwa mwingine mwenye udhuru ni, Wakili Alex Mgongolwa ni
mgonjwa ameshindwa kufika mahakamani kuendelea na kesi hiyo kwamba ni
busara Mahakama ikapanga tarehe nyingine ili kusikiliza rufani pamoja na
maombi ya dhamana.
Upande
wa Jamhuri ukiongozwa na Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini, Osward
Tibabyekomya akisaidiana na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Awamu Mbaga
na Theophil Mutakyawa, alidai kuwa hana pingamizi na ombi la utetezi.
Mbali na Dk. Lamwai, mawakili wengine wa utetezi ni, Dk. Ringo Tenga, Misangi Nzerahula, Godwin Nyaisa na Alex Mshumbusi.
Jaji
Mkasimongwa alisema baada ya pande zote mbili kukubaliana kuahirisha
kesi hiyo, Mahakama yake itasikiliza rufani pamoja na maombi ya dhamana
Julai 29, mwaka huu.
Awali
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu,
Emmilius Mchauru, ilifuta shtaka la nane la kutakatisha fedha dhidi ya
washtakiwa.
Hata
hivyo, upande wa Jamhuri ulikata rufaa kupinga uamuzi wa kuliondoa
shtaka hilo kwamba haukuridhika na uamuzi uliotolewa na Hakimu Mchauru.Hoja nyingine, Hakimu Mchauru alikosea kusema hati ya mashtaka ina dosari wakati siyo kweli.
Hoja
ya tatu, upande wa Jamhuri unaeleza kwamba uliomba nafasi kwa kuwa
kifungu cha 234 kidogo cha (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai
(CPA), hakimpi hakimu madaraka ya kuruhusu kubadilisha hati kama kweli
mahakama iliona ina dosari za kisheria.
Mbali
na Kitilya, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ambao wote wanasota
rumande ni aliyekuwa Miss Tanzania mwaka 1996 Shose Sinare na
mwanasheria wa Benki ya Stanbic, Sioi Solomon. Washtakiwa
hao walipandishwa kizimbani hapo kwa mara ya kwanza Aprili mosi, mwaka
huu, wakikabiliwa na mashitaka manane likiwemo la kutakatisha fedha Dola
za Marekani milioni 6 mali ya Serikali.
