Siku
mbili baada ya Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dk. Tulia Ackson kuagiza wabunge wa upinzani wanaoingia Bungeni na
kisha kuondoka wakisusa vikao wasilipwe posho, wabunge hao wamejibu
wakiubeza na kuupinga uamuzi huo.
Wakiongea
kwa nyakati tofauti, wabunge wa upinzani wamekosoa uamuzi huo wakieleza
kuwa Dk. Tulia alihukumu kesi inayomhusu, kitendo walichosema sio haki.
Aidha,
wabunge hao walieleza kuwa posho haitakuwa sababu ya kuwarudisha nyuma
kwenye uamuzi wao kwakuwa sio hoja wanayoipigania. Walisisitiza kuwa
wataendelea kutoshiriki vikao vya Bunge vinavyoongozwa na Dk. Tulia kama
walivyoazimia.
“Ukawa
haiwezi kutishiwa posho tunapokuwa na hoja na mawazo ya msingi. Hoja
yetu hapa si posho, kuna mambo ambayo anayafanya Naibu Spika hayaendi
sawa na sio ya kawaida. Hoja ya posho akawatishie watoto, sisi ni watu
wazima. Tumekuja hapa tuna utashi mkubwa,” alisema Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema).
Naye
Mbunge wa Vunjo na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema
kuwa uamuzi wa Naibu Spika unawadhalilisha wabunge kwa kuonesha kuwa
posho ndio kitu walichokifuata Bungeni hapo.
“Mimi
nimekuwa kwenye siasa kwa miaka zaidi ya 25 sasa. Kilichofanywa na
Naibu Spika ni kudhalilisha wabunge, ionekane sasa tupo hapa kwa ajili
ya kulipwa posho. Tupo hapa kwa ajili ya kutoa huduma kwa Watanzania.
Kina Tulia wakiwa shule ya msingi, sisi tunapambana bila kulipwa posho
na mtu yoyote,” alisema Mbatia.
Kiongozi
wa Kambi rasmi ya upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alitoa msimamo wa
kambi hiyo kuwa hawatashiriki vikao vyote vya Bunge vinavyoongozwa na
Naibu Spika kwakuwa amekuwa wakiwakandamiza na kupendelea upande mmoja.
Pia, Mbowe alisema kuwa Dk. Tulia anaongoza Bunge kwa ubabe akilinda
maslahi ya Serikali.