Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekabidhi shilingi Bilioni 12 kwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, zilizobaki
baada ya uchaguzi mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais uliofanyika tarehe
25 Oktoba, 2015.
Mwenyekiti
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damian Lubuva amekabidhi
hundi ya kiasi hicho cha fedha kwa Rais Magufuli leo tarehe 07 Juni,
2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa bakaa ya fedha hizo
haikuathiri kwa namna yoyote uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
"Mheshimiwa
Rais fedha ambazo tunakukabidhi, tulijibanabana sana, japo muda wenyewe
ulikuwa mfupi lakini tulijibanabana sana bila kuathiri utendaji wa
shughuli za uchaguzi, isije ikawa inatoa sura kwamba iliathiri,
haikuathiri, na katika hali hiyo kama ambavyo wengi ni mashahidi,
hatujisifii, lakini uchaguzi ulienda vizuri" Amesema Jaji Mstaafu Lubuva.
Akizungumza
baada ya kupokea mfano wa hundi hiyo, Rais Dkt. John Pombe Magufuli
ameipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuokoa fedha hizo na
kuzirejesha serikalini ili zipangiwe majukumu mengine na ametaka taasisi
nyingine za serikali ziige mfano huo wa uzalendo na kutanguliza maslahi
ya taifa.
"Kitendo
hiki ambacho mmekionesha leo, kinaonesha ni kwa namna gani Tume ya
Taifa ya Uchaguzi chini ya uongozi wako Mheshimiwa Mwenyekiti ilivyo na
watu makini na waadilifu sana, kwa sababu hizi fedha ambazo kwa lugha
uliyotumia ni bakaa, kutokana na zile ambazo mlipewa zaidi ya Shilingi
Bilioni 270, mkatumia shilingi Bilioni 261.6, mkabakiza shilingi Bilioni
12, mngeweza kuamua kusema hamkubakiza na hakuna mtu yeyote ambaye
angewauliza, na saa nyingine pengine hakuna mtu yeyote ambaye angejua,
mngeweza pia kusema kiasi mlichotupa hakijatosha, tunaomba mtuongezee
ama mngetengeneza maneno mazuri mazuri ya matumizi, bado nina uhakika
serikalini wasingejua" Amesema Rais Magufuli.
Pamoja
na kukabidhi hundi ya bakaa ya shilingi Bilioni 12, Mwenyekiti wa Tume
ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Mstaafu Damian Lubuva amemuomba Rais Magufuli
aisaidie tume hiyo kupata jengo lake la ofisi kwa kuwa hivi sasa tume
inatumia majengo ya kupanga ambayo yanaigharimu tume hiyo takribani
shilingi Bilioni 1 na Milioni 400 kila mwaka kwa kulipia kodi ya pango,
usafiri na gharama nyingine za uendeshaji.
Rais
Dkt. John Pombe Magufuli amelikubali ombi hilo na kuamua kuwa fedha
ambazo Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeziokoa (Shilingi Bilioni 12) kutoka
kwenye Uchaguzi Mkuu wa Mwaka jana zitumike kujenga ofisi ya tume, na
amependekeza ofisi hiyo ijengwe mkoani Dodoma.
"Na
mimi ningefurahi zaidi kama hilo jengo lingejengwa Dodoma, kwa sababu
Dodoma ndio makao makuu ya nchi hii, na hasa kwa sababu Dodoma ni
katikati ya Tanzania" Amesisitiza Rais Magufuli.
Rais
Magufuli pia amelikubali pendekezo la tume hiyo la kuanzishwa kwa mfuko
wa tume ya uchaguzi ambao utakuwa unakusanya fedha kila mwaka kwa ajili
ya uchaguzi mkuu unaofuata, badala ya kuendelea na utaratibu wa sasa wa
kusubiri mwaka wa uchaguzi ndipo zitengwe fedha zote za kugharamia
uchaguzi huo.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es Salaam
07 Juni, 2016