Mjadala wa bunge kuhusu bajeti umezidi kupamba moto baaada
ya wabunge wa Chama Cha Mapindunzi CCM kutumia muda huo kuwasema
wale wa upinzani na kulaani kitendo cha wao kutoka nje ukumbi hatua
ambayo inasababisha washindwe kuonyesha ushiriki wao katika bajeti
hiyo ambayo ni dira muhimu kwa taifa kwa mwaka 2016/2017.
Wakitumia dakika tano tano kwa kila mmoja wabunge hao akiwemo
Mh Livingstone Lusinde Mbunge wa Mtera wamesema kitendo cha wenzao wa
upinzani kususia mjadala huo hakileti afya kwa wananchi wa majimbo
wanayoyawakilisha na hivyo watizame upya maamuzi yao
Ushauari huo unakataliwa na Mh Joseph Mbilinyi mbunge wa
Mbeya mjini ambaye anasema wao wanaamini kuwa kuwawakilisha wananchi
siyo lazima kuingia bungeni na ndio maana hata sasa wanafanya vikao
vyao vya kuijadili bajeti hiyo katika ukumbi wa zamani wa msekwa
na watatumia mbinu zao wanazozijuwa kuwafikishia wananchi wao
taarifa za bajeti hiyo.
Hata hivyo kutokana na mvutano huo naibu spika Dk Tulia
Ackson analitolea ufafanuzi suala hilo ambapo anasema wabunge wa
upinzani kutoka nje wanafanya hivyo kwa utashi wao.
Katika hatua nyingine wakichangia hotuba hiyo Mh Ahmed Shabiby
mbunge wa Gairo amesema kwa sasa hali ya fedha mtaani ni ngumu
sana hivyo mpango wa serikali wa kuelekeza fedha zote hazina utazidi
kuongeza machungu huku Mh Oran Njeza mbunge wa Mbeya vijijini
akitaka ofisi ya CAG kuja na mkakati mpya wa kudhibiti fedha za
umma.