Manispaa ya Kinondoni, imewasimamisha kazi maofisa watendaji sita,
wakiwamo wanne wa kata na wawili wa mitaa kwa tuhuma za ubadhirifu wa
zaidi ya Sh400 milioni.
Kati yao, watendaji wawili wa kata na mmoja wa mtaa wameshafukuzwa kazi, huku manispaa ikiendelea na uchunguzi.
Uamuzi
huo ulitangazwa jana na Meya wa Manispaa hiyo, Boniface Jacob wakati
akizungumza na maofisa watendaji wa kata 34 za manispaa yao.
Jacob
aliyeambatana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Ally Hapi aliwataja waliofukuzwa
kazi kuwa ni Ernest Missa, Ally Bwamkuu na Aneth Lema.
Waliosimamishwa
kazi ni Shaaban Kambi, Dustan Kikweshi na Richard Supu ambaye alikuwa
anakaimu nafasi ya ofisa mtendaji wa kata.
“Hii ni aibu, Sh38
milioni hazionekani halafu meya yupo, kwa hali hii tutaoneana huruma
kweli, sasa hivi hakuna kuchezeana ni muda wa kufanya kazi.
“Najua
mtandao huu upo hadi makao makuu ya wilaya, ila niwaambie sasa hivi
ukisimamishwa utahojiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama
itakayowashirikisha Takukuru na ukibainika unapelekwa mahakamani na
Baraza la Madiwani linakufukuza kazi,” alisema Jacob.
Alifafanua
kwamba kati ya fedha hizo Sh400 milioni kila mtendaji anadaiwa kutumia
kiwango tofauti kwa nyakati tofauti, jambo ambalo linasababisha mgawanyo
wa fedha kutofika ngazi ya chini kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
“Ndiyo
maana kila siku migogoro kati ya wenyeviti wa mitaa na maofisa
watendaji haiishi, tatizo mojawapo ni hili. Tutaikomesha,” alisema
Jacob.
Jacob alitumia nafasi hiyo kuwaagiza watendaji kukusanya
kodi kwa ufanisi ili manispaa hiyo ifikie lengo la kukusanya Sh47
bilioni, kati ya Januari hadi Juni kutoka Sh39 bilioni ambazo
zimekusanywa hadi sasa.
Alizitaja baadhi ya kata zilizoko nyuma
katika ukusanyaji wa mapato kuwa ni Mburahati, Kibamba, Kimara, Mabibo
na Mabwepande huku na kata za Msasani na Sinza zikiongoza katika
ukusanyaji.
Mwenyekiti wa maofisa watendaji kata, John Njunde alisema maagizo yote watayafanyia kazi.
Mwenyekiti
wa watendaji wa Mitaa, Suleiman Sangongh’o alisema mkutano huo
unaowashirikisha viongozi wakuu wa manispaa unasaidia kuleta maendeleo
ya halmashauri hiyo.