Serikali imerasimisha jumamosi ya kila mwisho wa mwezi kuwa ni siku
ya usafi kitaifa kupitia sheria ya mazingira ya mwaka 2004 kifungu 191
ambapo mtu yeyote atakayekaidi kufanya usafi siku hiyo atatozwa faini
isiyopungua shilingi elfu hamsini au kifungo cha kuanzia miezi mitatu
mpaka miaka saba na atakayebainika kutupa taka hovyo atatozwa shilingi
laki mbili papo hapo na kwa kampuni au taasisi italipa milioni tano na
kuendelea.
Akitangaza kurasimishwa kwa siku hiyo katika zoezi la usafi wa
lililofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Naibu waziri ofisi Makamu wa
Rais Muungano na mazingira Mhe Luhaga Mpina amesema serikali imeridhia
iwe maalum kwa ajili ya usafi ambapo utekelezaji wake utasimamiwa na
viongozi kuanzia ngazi za chini kupitia muongozo wa tangazo la serikali
kupitia gazeti lake namba 139/2016 la tarehe 23 aprili mwaka huu.
Awali zoezi hilo almanusura liingie dosari ambapo wanafunzi
wanaosomea astashahada ya ualimu kumvamia waziri Mpina wakidai
hawajafundishwa kwa muda wa mwezi mmoja kufuatia mgomo wa walimu na
kumzuia waziri huyo kufanya kilichompeleka wakidai mpaka afike waziri wa
elimu sayansi na teknolojia Profesa Joyce Ndalichako kusikiliza madai
yao.
Kufuatia hali hiyo hali ikamlazimu waziri Mpina na baadhi ya
wabunge alioambatana nao akiwemo mwenyekiti wa kamati ya bunge ya
viwanda biashara na mazingira ambaye pia ni Mwalimu wa nje wa chuo hicho
Mhe Dalali Kafumu kutuliza hali ya hewa kwa kuwaahidi wanafunzi hao
kulifikisha suala hilo pahala husika.