Ikiwa bado kuna sintofahamu ya chanzo cha mauaji ya dada yake bilionea
Erasto Msuya, Anneth, Polisi wamesema hawajabaini sababu za awali za
kifo hicho na wanaendelea na msako wa waliohusika.
Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Temeke, Gilles Muroto alisema hadi jana wauaji walikuwa
hawajakamatwa, licha ya juhudi za upelelezi zinazoendelea.
Tukio
la Anneth Msuya aliyeuawa Alhamisi usiku kwa kuchinjwa nyumbani kwake
Kibada, Kigamboni jijini Dar es Salaam, limekuwa ni mwendelezo wa
matukio mengine ya uhalifu kwa familia yao yaliyowahi kutokea baada ya
kifo cha kaka yake, Msuya.
Miongoni mwa wanaotafutwa na Polisi
ni mfanyakazi wa ndani aliyeondoka nyumbani kwa Anneth mchana kabla ya
kutokea mauaji hayo, kwa madai kuwa hawezi kuendelea na kazi na kuacha
ufunguo kwa jirani.
Bilionea Msuya aliuawa Agosti 2012 kwa kupigwa risasi, tukio lililofanyika mkoani Kilimanjaro.
Ikiwa ni miaka minne tangu kifo hicho, kingine kinatokea kwenye familia hiyo.
Dada
wa Anneth, Ester, anayeishi Mbezi Makonde jijini Dar es Salaam, alisema
juzi kuwa mazishi ya mdogo wake yatafanyika mkoani Kilimanjaro Mei 30.
Bado
watu wengi wanajiuliza kuhusu mfululizo wa matukio katika familia ya
Msuya, huku wakishangaa sababu za binti huyo kuuawa kama kaka yake.
“Ni
kweli kifo hupangwa na Mungu, lakini siyo kwa kifo hiki. Kwa nini
wanauawa?” alihoji Juma Majuto, mmoja wa waombolezaji wa msiba huo
uliopo Mbezi Makonde.