Polisi mkoani Mara inamshikilia mganga wa
zahanati katika Kijiji cha Rwamchanga wilayani hapa kwa madai ya kushindwa kumhudumia mjamzito aliyejifungua mapacha na kusababisha kifo mtoto mmoja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Ramadhan Ng’anzi
amesema tukio hilo lilitokea Mei 15.
“Tunamshikilia kwa makosa matatu, likiwamo la uzembe, kufanya makusudi na kushindwa
kuwajibika sawa na kiapo cha kazi yake, tunaendelea na mahojiano yatakapokamilika atafikishwa mahakamani,” amesema Ng’anzi.
Akisimulia chanzo cha mwanae kupoteza maisha, Shida Mugesi akiwa katika Hospitali ya Nyerere
alisema alifika hospitalini saa 12 asubuhi na kumuomba mganga amuhudumie, lakini alikataa.
“Nilikaa kwa muda wa saa mbili bila kupatiwa huduma, ghafla nilihisi uchungu wa kusukuma mtoto tukamuita mganga wa zamu ili anisaidie aligoma na kudai nimsubiri anakwenda kuoga na
wakati huo alikuwa anazungumza kwa simu bila kuonyesha ushirikiano.
Baada ya kugoma
kunisaidia nilianza kujifungua mwenyewe,” alisema.
Muuguzi ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema walipopima uzito wa watoto kwa mjamzito
huyo walibaini kuwa aliyefariki alikuwa na kilo 2.5 na mwingine 2.3.
Muuguzi wa zahanati hiyo, Frida Kasonga alisema aliposikia taarifa ya kuwapo kwa mgonjwa huyo
alilazimika kurudi kituoni kumsaidia lakini alikuta mtoto mmoja ameshafariki dunia.
“Haikuwa zamu yangu ila nililazimika kurudi baada ya kusikia mganga aliyekuwa zamu kagoma
kuwasaidia,” alisema Frida.
Ofisa mtendaji kata, Fdhila Nyamburapi na Mwenyekiti wa kitogoji cha Kazi, Samwel Nyakande
walilaani kitendo hicho na kutaka sheria ichukue mkondo wake.
