Mwanamke
huyo, ambaye jina lake halijapatikana, alipelekwa na mumewe kwenye
zahanati hiyo usiku baada ya kupatwa uchungu, lakini alipofika wauguzi
hao waliona kuwa anachelewa kujifungua. “Waliamua kumuita mumewe na
kumvisha gloves (mipira ya kujikinga), kisha wakaondoka,” alisema
mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Kalolo Joseph Ntila
na kuongeza: “Usiku mzima mume alifanya kazi ya kuhangaika na mke wake
na waliporudi asubuhi, wakakuta mama anajifungua, mtoto akiwa amechoka
na akafariki dunia.
“Kwa
hiyo tumeunda kamati wakati wao wakiwa nje kwa muda kupisha uchunguzi
na ikibainika wana makosa tutawachukulia hatua zaidi.” Mwenyekiti wa
halmashauri hiyo hakuweza kukumbuka jina la mjamzito huyo na mumewe na
juhudi za kuwapata wawili hao hazikuzaa matunda. Katika tukio jingine;
halmashauri hiyo imewasimamisha kazi wauguzi na madaktari wasaidizi wa
zahanati za vijiji vya Uzia, Muze na Mpui kwa tuhuma za uzembe na
kusababisha vifo ya wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka
mitano. Awali, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Adam Missana
alisema watumishi wengine wanne wamefukuzwa kazi wakiwamo mafundi,
wahudumu wa maabara, wauguzi na wahudumu wa afya kutokana na utoro
kazini.
Taharuki
Hospitali ya Temeke Hali ya sintofahamu jana asubuhi iliikumba
Hospitali ya Temeke baada ya wakaguzi kufika kufanya uhakiki wa
watumishi hospitalini hapo na kusababisha wagonjwa kutelekezwa kutokana
na wauguzi kufuata vyeti majumbani mwao.
Maeneo
yaliyoathirika na purukushani hiyo ni pamoja na upande wa huduma kwa
wazee, wajawazito, wagonjwa wa kawaida na katika baadhi ya wodi. Mkuu wa
Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliagiza wakuu wa wilaya zake
kuacha masuala mengine na kujikita kwenye ukaguzi wa watumishi hewa
kwenye sekta zote.
Mgonjwa
aliyekutwa hospitalini hapo, Monica Kessy alisema daktari aliyekuwa
akiwahudumia aliondoka, hivyo kuwalazimu wagonjwa kupanga foleni kwa
daktari mmoja pekee. “Ilipofika saa 5:00 hivi tukaona wanatoka na kukaa
vikundi vikundi wakielezea kuna uhakiki. Wengine wakaanza kuondoka.
Baadaye tukasikia tangazo kuhusu uhakiki, manesi na madaktari wengi
wakaondoka,” alisema Monica.
“Usipowasilisha
vyeti utaonekana wewe mtumishi hewa, hivyo katika kuliepuka hilo kila
mmoja anatetea ugali wake. Masjala hatuwezi kutosha mule, wengine
tukarudi majumbani mwetu kuchukua vyeti,” alisema mmoja wa wauguzi
ambaye hakupenda kutaja jina. Mganga mkuu wa hospitali hiyo, Dk Amani
Malima alisema hitilafu hiyo imetokana na uhakiki wa watumishi ambao
unaendelea kufanyika hospitalini hapo.
“Huduma
zinaendelea si kusema kwamba imesimama. Watumishi walitangaziwa tangu
jana kutakuwa na uhakiki mwingine. Kazi lazima iendelee,” alisema.
chanzo: MWANANCHI
