WAWEKEZAJI na wafanyabiashara wakubwa na wadogo wilayani Muheza mkoani Tanga ambao watagoma kuchangia fedha za maandalizi ya ujio wa Mwenge wa Uhuru katika wilaya hiyo wafungashe vilago kwani watakuwa hawafai
Hayo yalisemwa juzi na mkuu wa wilaya ya Muheza Esterina Kilasi katika kikao cha cha maandalizi ya ujio wa Mwenge wa uhuru wilayani Muheza kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa halmashauri ya wilaya ya Muheza na kushirikisha wakuu wa idara, watendaji wa kata, maafisa tarafa na viongozi wa vyama vya siasa.
Alisema mwenge wa uhuru ni kitu muhimu katika nchi hii toka enzi ya Baba wa Taifa hayati Julius Kambarage Nyerere, kwa hiyo alisema wafanyabiashara lazima wachangie pamoja na wafanyakazi na watu binafsi ili kuongeza nguvu
katika ujio wake huku akimuagiza afisa biashara wa wilaya kuorodhesha wafanyabiashara wote ambao hawana leseni ili wachukuliwe hatua.
Kilas alisema kama mwekezaji hataki kuchangia mwenge wa uhuru, aondoke katika wilaya yake kwa kuwa atakuwa hafai kwani mwenge wa uhuru unaunganisha watu kuwa pamoja na kuleta maendeleo ya kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aliwataka maafisa watendaji wa kata na Afisa biashara wa wilaya hiyo kukusanya fedha hizo za maandalizi ya ujio wa mwenge wa uhuru ambao utawasili wilayani Muheza Tarehe 2/5/2016 ambapo utazipitia miradi mbalimbali ya maendeleo katika halmashauri hiyo.
Mkuu huyo wa wilaya alisema mwenge huo wa uhuru utapokelewa kimkoa katika wilaya ya Kilindi ukltokea mkoa wa Morogoro tarehe 25/4/2016 ambapo utaelekea wilayani Handeni, hadi Korogwe vijijini, utaelekea pia wilaya ya Korogwe mjini, halafu Bumbuli, Lushoto mjini, wilayani Mkinga,wilaya ya Muheza,wilaya ya Pangani na kumalizikia wilaya ya Tanga mjini na baada ya hapo utakwenda Pemba.
Alisema katika wilaya ya Muheza, Mwenge huo utawasili saa tatu asubuhi ukitokea wilayani Mkinga na utapokelewa katika kijiji cha Mjesani kata ya Mjesani wilayani Muheza ambapo utapitia miradi saba mwaka huu wa 2016 katika wilaya hiyo na kauli mbiu ya mwenge wa uhuru mwaka 2016 inaseama, 'Vijana ni Nguvu kazi ya Taifa Washirikishwe na Kuwawezesha'.
kwa upande wake mratibu wa mbio za Mwenge wilaya ya Muheza, Mboza Singa aliitaja miradi ambayo itapitiwa na mwenge wa uhuru katika wilaya hiyo kuwa ni kuweka jiwe la msingi vyumba vya madarasa shule ya sekondari
Pande darajani, kuweka jiwe la msingi mradi wa maji kijiji cha Upare tarafa ya Ngomeni, kukagua mradi wa ufugaji kuku katika kijiji cha Muungano,
Miradi mingine kuweka jiwe la msingi ofisi ya kijiji cha Kwemkabala,kukagua mradi wa wanawake kijiji cha Mlingano,kukagua mradi wa vijana wauza nguo za mitumba kata ya Tanganyika na kukagua nyumba wa sekta
binafs ya kulala wageni katika kata ya Genge miradi hiyo iliwa na thamani ya makisio ya bilioni 2.5/-.