Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya Gairo
wamesema hawaridhishwi na utendaji kazi wa mkurugenzi wa
halmashauri hiyo, Mbwana Magota kutokana na kutoitisha
vikao halali vya madiwani na kushindwa kusimamia kwa
usahihi fedha za miradi.
Wakizungumza baada ya kuahirishwa
kwa kikao maalum cha baraza la madiwani, madiwani hao
walisema kuna miradi ya ujenzi barabara imetekelezwa katika
kiwango duni na imeshaharibika ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Rahel Nyangasi aliwaambia waandishi wa habari kuwa kwa muda mrefu wameomba kufanya ziara ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa katika halmashauri hiyo lakini mkurugenzi hataki kuwapeleka.
“Kikao cha leo tuliitisha wenyewe madiwani na agenda zilikuwa kujadili mustakabali wa
halmashauri yetu kwani mkurugenzi amekua haitishi vikao na tuna kero nyingi za wananchi za
kujadili na hatujui tutazijadili wapi wakati hakuna vikao”
Vikao ambavyo wanalalamikia madiwani hao ni vikao vya kamati za halmashauri ambavyo
vinatakiwa kufanyika mara moja kila mwezi na kikao cha baraza la madiwani ambacho hufanyika mara moja kila baada ya miezi mitatu.
Wakati akiahirisha mkutano huo Mwenyekiti huyo aliwaambia madiwani kuwa wamekiuka
taratibu za kuitisha kikao kwani kabla ya kikao hicho walitakiwa watume barua kwa mkurugenzi
ya kuitisha kikao ikiwa imesainiwa na theluthi moja ya madiwani wote jambo ambalo
halikufanyika.
