NAPE Nnauye, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo amesema, hatoacha kutilia fitina maofisa habari wa serikali ambao hawashirikiani na waandishi wa habari katika kuwapa taarifa
Amesema, endapo watashindwa kutoa ushirikiano kwa waandishi wa habari, wataondolewa kwenye nafasi hizo.
Nnauye ambaye pia ni Katibu wa Siasa, Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amesema hayo leo wakati akifungua kikao cha kazi cha maofisa mawasiliano wa serikali katika Ukumbi wa VETA, Morogoro.
Amesema, yapo malalamiko mengi ya maofisa habari kuwaogopa ama kuwakimbia waandishi wa habari pale wanapotaka kupata taarifa jambo ambalo amedai kukwamisha upatikanaji wa taarifa kwa umma.
‘’Sitaacha kutia fitina kwa ofisa habari anayekimbia wandishi wa habari ili abadilishwe kazi, unakuta kitu kidogo anawazungusha waandishi wa habari, njoo kesho, kesho kutwa wakati angeweza kutoa taarifa kwa wakati,’’ amesema.
Aidha amewataka kujenga uhusiano mazuri na vyombo vya habari ili kuwezesha upatikanaji wa habari za maendeleo ya nchi kutoka serikalini kwenda kwa umma.
Pia ameagiza vitengo vya mawasiliano viandae mkakati wa mawasiliano kwa umma utakaotekelezeka, ambapo kila taasisi ya serikali ionekane inajitangaza kwa umma kimkakati kupitia Radio, Televisheni, Magazeti na mitandao ya kijamii.
Amesema kwa kutekeleza majukumu yao kisasa kwa kuzingatia karne iliopo ya sayansi na teknologia, hivyo tovuti za serikali ziwekwe taarifa sahihi kwa wakati, sambamba na kutumia mitandao ya kijamii kutoa taarifa za serikali na kupokea taarifa ambazo watazifanyia kazi.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo Profesa Elisante Gabriel amesema, changamoto kubwa inayowakabili maofisa hao ni pamoja na kutothaminiwa katika maeneo yao ya kazi, sambamba na uhaba wa bajeti pamoja na vitendea kazi.
Mkurugenzi wa Tanzania Association of Government Communication officers (TAGCO) Innocent Mungi amesema, upo umuhimu kwa sasa maofisa hao kushirikia vikao vya menejimenti katika maeneo yao ya kazi badala ya kupewa taarifa tu badaa ya vikao kwaajili ya kuzitoa katika vyombo vya habari.
‘’ Unakuta menejimenti inakaa yenyewe bila afisa mawasiliano, alafu anakuja kupewa taarifa tu hivyo ikitokea hoja ya kuitolea ufafanuzi zaidi inakuwa vigumu kwake’’ amesema.