SERIKALI imeanzisha mfumo wa Kielektroniki wa malipo ya mishahara kwa watumishi wa umma ambao unalenga kuondoa tatizo la madai ya malimbikizo ya stahili zao.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana (Jumamosi, Machi 5, 2016) wakati akizungumza na watumishi wa sekta mbalimbali katika wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu.
Waziri Mkuu alisema mfumo huo ujulikanao kama LAWSON, unatumika kwenye ajira za watumishi wote nchini, wa Serikali Kuu na wale wa Serikali za Mitaa
Waziri Mkuu alisema mfumo huo unasaidia kutunza, kutuma na kuhuisha taarifa za watumishi kwa wakati na kwa ufanisi tangu mtu anapoajiriwa hadi inapofikia wakati wa kupandishwa madaraja na hadi anapostaafu.
Kabla ya kuanzishwa kwa mfumo huo, maafisa utumishi walipaswa kukusanya taarifa za watumishi wote walioajiriwa na kuzipeleka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma ili zikathibitishwe kabla ya kuzipeleka HAZINA kwa maandalizi ya mishahara.
Akitolea mfano wa kada ya ualimu, Waziri Mkuu alisema ajira za walimu zilikuwa zinaanzia Idara ya Utumishi wa Walimu (TSD) lakini anapaswa aende kuripoti kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri (DED) ambaye ni mwajiri wake chini ya TAMISEMI.
"Hii ilileta ugumu wa malipo ya kupanda madaraja, uhamisho ama likizo kwa sababu mwajiri anakuwa hajatenga hizo fedha."
"Sasa hivi tuna Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) ambayo iko chini ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri. Kwa hiyo ni rahisi wao kukaa pamoja na kuamua tuwapandishe daraja walimu 10 na wote hao wakalipwa bila bila kuchelewa," alisema.
Alisema mfumo huo umeanza kutumika tangu mwaka 2012 na ulianza kwa ajira mpya za walimu na hadi sasa umethibitisha kuwa inawezekana kumlipa mtumishi mshahara wake hata kama ameajiriwa ndani ya mwezi huohuo.
"Kama mtumishi anaripoti kwenye kituo kipya hata iwe wilaya ya wapi ili mradi amefika na barua zake zote na ziko sahihi mtu huyu ataingiziwa taarifa zake na wakati huohuo taarifa zitaonekana Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na pia zitapokelewa kwa maafisa wanaoshughikia mishahara kule HAZINA."
Alisema changamoto pekee waliyokutana nayo wakati mfumo huo umeanza ilikuwa ni kutoingizwa taarifa za wale ambao wameripoti baada ya tarehe 10 ya mwezi husika.
"Hii ni kwa sababu matayarisho ya mishahara yanakuwa yameshaanza. Kwa hiyo wengi walishauriwa kuripoti kati ya tarehe 25 hadi tarehe 9 ya mwezi uliofuata na wote hawa hawakupata matatizo ya kucheleweshewa mshahara," alisema.
Akifafanua kuhusu upandishaji madaraja ya watumishi, Waziri Mkuu alisema Serikali imeondoa utaratibu wa mtumishi kulazimika kuandika barua ya kukiri kupandishwa daraja/cheo ndipo aanze kupata stahili zake mpya.
"Hii imeondoa ucheleweshaji wa kufanyika marekebisho ya mshahara na pili imeondoa tofauti za mishahara kwa watumishi wenye ngazi moja (sifa sawa za kitaaluma, tarehe moja ya kuajiriwa) ambao walikuwa wakilipwa tofauti kwa sababu mmoja aliwahi kuandika barua ya kukiri na mwingine alichelewa kuandika barua hiyo hiyo " alisema
AKATISHA ZIARA KUTOKANA NA MSIBA
Wakati huohuo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amelazimika kukatisha ziara ya mkoa wa Simiyu ambayo ilikuwa imalizike kesho kutokana na msiba wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ambayo alipangiwa kuitembelea leo.
Mkurugenzi huyo Bw. Traceas Kagenzi alifariki dunia usiku wa kuamkia jana kutokana na shinikizo la damu. Atasafirishwa kwenda Muleba kwa mazishi.
Akitoa salamu za rambirambi kwenye ibada ya kumuombea marehemu Kagenzi iliyofanyika nyumbani kwake Maswa mjini, Waziri Mkuu alisema ameshtushwa na msiba huo uliotokea ghafla na kwamba Taifa limempoteza mtumishi mahiri ambaye bado Taifa lilikuwa likimtegemea.
"Nimeshtushwa sana na taarifa za msiba huu. Nimeambiwa hadi juzi usiku alikuwa akishirikiana na Mkuu wa Wilaya hii kuandika taarifa ya ziara ya wilaya hii. Kwa niaba ya Serikali, ninawapa pole sana wafiwa na Mungu awape uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi,"alisema.
"Nimelazimika kukatisha ziara ya mkoa huu kwa sababu huyu ni mtumishi mwenzetu" alisema Waziri Mkuu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, MACHI 6, 2016.