Uongozi mkoani Mbeya umeifunga Shule ya Sekondari Iyunga baada ya mabweni matatu kuungua moto na wanafunzi kulala nje kutokana na kuyaogopa mabweni yaliyobaki.
Kwa kawaida likizo fupi ilitakiwa kuwa kipindi cha pasaka, lakini shule hiyo ilifungwa Machi 11 hadi 25 na kwamba itaendelea kufungwa hadi Aprili Mosi.
Mkuu wa shule hiyo, Edward Mwantimwa alitoa maelezo hayo kwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jaffo aliyefika shuleni hapo juzi kujionea uharibifu uliotokana na moto uliounguza mabweni matatu kwa nyakati mbili tofauti.
Mwantimwa alisema mara ya kwanza mabweni ya Nyerere na Mkwawa yaliungua Februari 29 na Machi 7 la Shaban Robert, jambo ambalo lilisababisha hofu kwa walimu na wanafunzi na kuanza kuyasusa mabweni mengine.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Nyirembe Munasa akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa alimueleza naibu waziri hatua zilizochukuliwa ikiwamo wadau kutoa misaada na kwamba, pia walikuwa wanaandaa harambee ambayo wangependa ifanyike Dar es Saalaam.
Jaffo alilitaja tukio hilo kuwa ni janga na kuahidi kuwashirikisha wabunge wote kuchangia kurudisha hadhi ya shule hiyo.
“Kuungua kwa shule hii kumeonyesha mengi yakiwamo ya uchakavu wa miundombinu,” alisema.
Alimtaka Nyirembe kusimamia ukarabati wa shule hiyo na uwe umekamilika ifikapo Aprili Mosi.