Nyumba ya Kamishna wa Polisi Zanzibar imelipuliwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu

Na Mwashungi Tahir na miza Kona – Maelezo Zanzibar    
Nyumba ya Kamishna wa Jeshi la Polisi Zanzibar Hamdan Omar Makame imeripuliwa  na kitu kinachosadikiwa kuwa  ni bomu na watu wasiojulikana  majira ya saa 5.00 usiku huko Kijichi nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari Ofisini kwake Makao Makuu ya Polisi Kilimani, Kamishna Hamdani amesema tukio hilo limeathiri sehemu ya paa la nyumba na dari na  kujeruhi baadhi ya watu  waliokuwa wamelala  na kusababisha hasara kubwa.

Amesema tukio hilo linafanana na  lile lililotokea tarehe 03 mwezi huu katika Maskani ya CCM Kisonge Unguja hivyo polisi inaendelea kufanya uchunguzi ikiwa ni pamoja na kuwasaka wahalifu wanaofanya  uhalifu huo.

Akizungumzia  matukio  mengine ya uhalifu na kuchoma moto nyumba, maskani na kituo cha Afya huko Pemba, alisema  Jeshi la Polisi limeanza msako mkali na kuwatia mbaroni watu 31 ambao wanaendelea kuhojiwa na watakaohusika watafikishwa  katika vyombo vya sheria.

Kamishna Hamdani amewatoa hofu  wananchi kuhusu usalama wao na mali zao kuelekea uchaguzi wa marudio utakaofanyika tarehe 20 mwezi huu na kuwepo kwa ongezeko la askari katika maeneo  mengi ya mijini na vijijini  ni  moja ya juhudi za kuimarisha  ulinzi  na kuhakikisha  uchaguzi huo utakuwa salama na amani.

Ametahadharisha kuwa mtu yoyote atakayejihusisha kuanzisha vurugu au kufanya kitendo chenye ishara ya  uvunjifu wa amani atapambambana na vyombo vya sheria.

Kamishna Hamdani ametoa wito kwa wananchi waliojiandikisha kupiga kura kujitokeza kwa wingi siku hiyo ili waweze kutimiza haki yao ya msingi ya kikatiba bila ya woga  kwani jeshi hilo limejipanga  kuimarisha ulinzi  sehemu  zote.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo