Naibu Waziri wa TAMISEMI Suileman Jaffo amewapa siku nane viongozi wa Halmashauri ya jiji la Arusha kukamilisha ujenzi wa shule ya msingi Kisimani iliyokumbwa na upepo mkali ulioezua paa la shule hiyo jambo ambalo limesababisha wanafunzi kukosa mahali pa kusomea.
Aidha amemtaka Mkurugenzi wa jiji la Arusha Juma Idd na kamati yake kutoa maelezo ya sababu zilizochangia ukarabati wa shule hiyo kuchelewa na kwa nini hatua zisichukuliwe dhidi ya watendaji wenye dhamana ya kusimamia jambo hilo.
Naibu huyo ameuhoji uongozi wa jiji kwa kutokuchukua hatua muda mrefu bila kufanya ukarabati tangu tatizo hilo lilipotokea Disemba 4 mwaka jana na kusababisha wanafunzi kukosa sehemu nzuri ya kujifunzia.
Hata hivyo Jaffo amesema serikali haitavumilia uzembe unaofanywa na watumishi hususani katika maeneo yaliyokumbwa na maafa na kutoa wito kwa wakurugenzi kote nchini kutimiza majukumu yao.
Afisa Manunuzi wa Jiji la Arusha Seif Kasori amejitetea kwa kudai kwamba alichelewa kupata taarifa za manunuzi hali ilisababisha kuchelewa kwa ukarabati wa shule hiyo.
Naibu waziri amefanya ziara ya kushtukiza katika shule ya Msingi Kisimani na kujionea hali halisi,ambapo pia ametembelea hospitali ya Kaloleni pamoja na soko kuu la Arusha.