Wananchi wa kijiji cha Lupalilo kata ya Lupalilo wilayani Makete mkoani
Njombe wamekataa kuipokea taarifa ya mapato na matumizi ya kijiji hicho ya
Septemba hadi Desemba 2015
Wananchi hao wamefikia hatua hiyo baada ya kutokubaliana na matumizi ya
shilingi 201,000 yaliyotumika kwa ajili ya kushughulikia kesi ya kifusi pamoja
na wajumbe wa halmashauri hiyo kutumia zaidi ya shilingi laki tano kwa ajili ya
kujilipa posho
Baada ya majadiliano ya muda mrefu kwenye mkutano wa kijiji wananchi
walimuamuru mwenyekiti wa kijiji hicho ambaye baada ya muda alijiuzulu Bw.
Victoni Sanga kuzirudisha fedha hizo na wakati kijiji kikiwasomea taarifa ya
mapato na matumizi itakayofuata ambayo itasomwa mwezi Machi mwaka huu, fedha
hizo ziwe zimerudi
“jamani hivi hawa wajumbe tuliwatuma wakagawane posho au wasimamie
maendeleo ya kijiji chetu? Kwa kweli mwenyekiti mimi naona hawa wajumbe wa
halmashauri ya kijiji wapo kujinufaisha, haiwezekani watumie zaidi ya laki tano
kwa ajili ya posho tu hivi sisi tutaendelea lini jamani?” amesikika mwanamama
mmoja akizungumza kwenye mkutano huo bila kutaja jina lake
Pamoja na maamuzi hayo ya wananchi kaimu Afisa Mtendaji wa kata hiyo Bw.
Mwatima Mbiliyi amewaambia wananchi hao kuwa wajumbe wako sahihi kutumia kiasi
hicho cha fedha kwa ajili ya posho kwa kuwa kosa ni la kwao wananchi kutopanga
watumie shilingi ngapi kwa kila mjumbe katika vikao vyao
“Mimi nasema wajumbe wako sahihi kabisa kutumia kiasi hicho cha fedha, na
tena msiwalaumu kwa kuwa kosa ni lenu wananchi hamkuwapangia watumie shilingi
ngapi, sasa mnawalaumu kwa lipi? Japo mimi ni mgeni hapa Lupalilo lakini
nimejifunza kitu, ili kuondokana na yote haya mnatakiwa muwapangie kila mjumbe
apewe posho ya shilingi ngapi kwa kila kikao wanachokifanya” amesema Mbilinyi
Naye diwani wa kata hiyo Mh. Imani Mbilinyi amesema wananchi hao wapange
kiwango cha kulipwa wajumbe huku akitolea mfano katika kijiji cha Kisinga
ambacho kipo katika kata yake kuwa wamepanga kila mjumbe alipwe shilingi 2,000
kwa kila kikao wanachokaa, jambo ambao limeondoa malumbano katika kijiji hicho
Mwananchi akielezea sababu za kukataa taarifa hiyo
Kaimu Afisa mtendaji wa kata ya Lupalilo Bw. Mbilinyi akisisitiza jambo kwa wananchi baada ya taarifa hiyo kukataliwa