Na Erica Mbilinyi.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Makete mkoani Njombe Mh.Egnatio Mtawa (pichani juu) amefanya ziara ya kushtukiza katika shule ya sekondari Iwawa wilayani Makete ili kujua mapokezi ya elimu Bure na changamoto ya mfumo huo.
Mara baada ya kufika shuleni hapo amekutana na mkuu wa shule hiyo Mwl.Antony Ng'wavi ambaye amesema licha ya uwepo wa changamoto ya uelewa mdogo wa wananchi juu ya michango wanayotakiwa kuitoa lakini wamekuwa wakiwaelimisha wazazi na walezi na kukubaliana kutoa michango ya chakula kwa watoto wanaoishi bwenini.
Diwani wa kata ya Iwawa Mh Asifiwe Luvanda.
Naye diwani wa kata ya Iwawa wilayani Makete Mh.Asifiwe Luvanda akiwa shuleni hapo alihoji ili kutaka kujua kuhusiana na utaratibu wa utoaji wa Risiti pindi wanafunzi wanapotoa michango mbalimbali kwa kuwa kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wanafunzi kutopewa risiti.
Akijibu hoja hiyo Mkuu wa shule ya sekondari Iwawa amesema kuwa risiti wanatoa licha ya changamoto ya kukosekana kwa mhasibu na kusema kuwa mwalimu ambaye anasimamia suala la malipo shuleni hapo amekuwa na kazi nyingi kwa wakati mmoja na kushindwa kuwahudumia wanafunzi wote kwa wakati mmoja.
Akikamilisha ziara yake katika shule hiyo ya sekondari mwenyekiti huyo wa halmashauri ya wilaya ya Makete ametoa wito kwa wazazi na walezi wote wilayani Makete kuunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali kwa kuendelea kuchangia chakula kwa matumizi ya watoto wao mashuleni.
