Majanga: Rais awakamata laivu polisi wakipokea Rushwa

POLISI wawili wa trafiki jijini Mombasa walisimamishwa kazi baada ya kupatikana peupe na Rais Uhuru Kenyatta wakipokea mlungula.
Rais Kenyatta jana alieleza jinsi alivyoshuhudia maafisa hao wakipokea hongo wakati alipokuwa katika ziara Pwani na akatoa onyo kali kwa wengine wanaopenda kuvuna wasikopanda kwamba wataadhibiwa.

“Juzi nilikuwa Mombasa, jamani mtu amesimamisha gari katikati (ya barabara) akichukua pesa kutoka kwa abiria.
“Sasa jamani wale wote ambao walikuwa nyuma, mimi nikiwa mmoja wao, na wanaona mtu akichukua pesa unadhani wanafikiria nini?,” akashangaa rais.
Alikuwa akizungumza katika kongamano lililoandaliwa na Inspekta Mkuu wa Polisi Joseph Boinnet, ambalo liliwaleta pamoja waratibu wa maeneo, makamanda wa kaunti na maafisa wengine wa ngazi za juu katika eneo la South C, Nairobi.
“Tuambiane ukweli, hatuwezi kudumu katika hali hiyo. Sitakubali kitu kama hicho kifanyike,” akasema.
Duru za kuaminika jana zilithibitisha kusimamishwa kazi kwa maafisa hao wawili, ingawa hakuna afisa wa polisi alitaka kufichua mengi kutokana na kuwa “rais tayari alikuwa amelizungumzia suala hilo”.
Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa maafisa hao walikuwa wakihudumu katika kituo cha polisi cha Makupa, na walikuwa wametiwa kizuizini kwa siku tatu kuanzia Januari 10, kabla ya kusimamishwa kazi.
Wawili hao walitambuliwa kama Koplo Barnaba Ruto na Konstebo Joel Atuti, na walipewa siku saba kukata rufaa.
Katika hafla ya jana, rais aliwahimiza polisi kuhakikisha kwamba wanazingatia haki za binadamu katika utekelezaji wao wa sheria, ili kuzuia kesi nyingi dhidi ya serikali pamoja na kudumisha imani ya umma ambayo ni muhimu kwao katika kufaulisha wajibu wao.
 Hata hivyo, rais aliwapongeza maafisa hao kwa wajibu waliotekeleza wakati wa ziara ya Baba Mtakatifu na Kongamano la Kimataifa la Kibiashara mwaka jana, kukabiliana na wizi wa mifugo na uvamizi katika eneo la kaskazini mashariki.

Wizi wa mifugo
“Aidha, mnahitaji kuimarisha juhudi zenu katika maeneo mengine kama ya mipaka ya kaunti za Meru na Isiolo, na maeneo ya kaskazini mwa Kaunti ya Samburu, yanayoendelea kushuhudia wizi wa mifugo,” alisema.
Alitangaza kuwa kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa hili, polisi watakuwa na magari yenye kinga za risasi, ambayo yatawasaidia kukabiliana na uhalifu na ugaidi nchini.
Alisema kuwa shughuli za polisi zinaendelea kuboreshwa na wanatarajia kupata helikopta mbili mpya kufikia Juni mwaka huu, huku nyingine mbili zilizopelekwa kukarabatiwa zikitarajiwa kurejeshwa zikiwa shwari.
Rais Kenyatta aliwataka makamanda wa polisi wawe katika mstari wa mbele kuwezesha kikosi hicho kujiondolea sifa mbaya za ufisadi na huduma mbaya kwa umma ambazo hutolewa mara kwa mara na mashirika mbalimbali ya utafiti.


JIUNGE NA EDMO BLOG SASA

Usipitwe!! Jiunge nasi kupitia Facebook,Twitter na Instagram ili kupata habari zote za town! Usikose kujiunga na Youtube kuangalia video zote kali kutoka Edmo Blog Pekee!, kujiunga bonyeza hapa>>>Youtube

Tupe Maoni Yako lakini Usiandike Matusi



 
© Copyright EDMO BLOG | Designed By Peruzibongo